SOMAFCO kujenga kiwanda cha korosho Tanzania

Muktasari:

Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha kuwezesha vijana kielimu na kiuchumi(SOMAFCO) limesema licha ya kuwekeza katika eneo la Morogoro, linatarajia kuanzisha viwanda mbalimbali vikiwemo vya kubangua korosho

Dar es Salaam. Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha kuwezesha vijana kielimu na kiuchumi (SOMAFCO) linatarajia kuanzisha kiwanda cha kubangua korosho mkoani Morogoro nchini Tanzania.

SOMAFCO itaanzisha kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono mahitaji ya Tanzania katika uwekezaji wa viwanda vya kuungua zao hilo.

Kauli hiyo imetolewa jana Alhamisi Agosti 15,2019 kupitia Mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara wa Nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mkuu wa SOMAFCO, TIholo Mohlathe amesema Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa zikishirikiana kwa kipindi kirefu tangu kupigania uhuru hivyo kwa sasa kituo hicho kitachochea ukuaji wa shughuli za uzalishaji wa zao hilo.

“Tunatarajia kuanzisha kiwanda hicho,  ushirikiano huu tunataka uendelee na tunataka kufanya kazi na viwanda vya mafuta Morogoro na kuendelea kutunza kumbukumbu za kihistoria, tunajua kuwa kupitia mradi wa SGR tutafanikiwa katika mengi,” amesema Mohlathe

Katika kipindi cha kupigania ukombozi kusini mwa Afrika, SOMAFCO kilikuwa ni chuo cha Wapigania Uhuru wa Afrika kusini cha Solomoni Mahalangu, mkoani Morogoro.

Baada ya kumalizika shughuli za ukombozi, SOMAFCO ilibakia kuwa ni kampasi ya chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine(Sua), kilichopo  Morogoro.