Saa 11 za vita mawakili wa Lissu, Serikali walivyochuana mahakamani asubuhi mpaka usiku

Mawakili wanaemtetea aliekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu  wakipitia nyaraka katika mahakama Kuu jijini Dar es Salam juzi.kutoka kulia ni  Peter Kibatala ,   Jeremiah Mtobesya  na  kushoto ni Omar Msemo . Picha na Omar Fungo

Muktasari:

  • Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema kufungua kesi ya kupinga ubunge wake kunahitaji umakini wa hali ya juu, na hilo lilijionyesha juzi mahakamani

Dar es Salaam. Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema kufungua kesi ya kupinga ubunge wake kunahitaji umakini wa hali ya juu, na hilo lilijionyesha juzi mahakamani.

Mawakili 14 wa Serikali walipambana na mawakili wanne wa Lissu kwa takriban saa 10: 28. Upande wa Serikali una kesi rejea 70 kukabiliana na kesi 50 za Lissu katika kesi hiyo inayofuatiliwa kwa karibu.

Kesi hiyo inatokana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai kufuta ubunge wa Lissu siku 58 zilizopita kwa maelezo kuwa hajulikani alipo na hakusaini fomu za maadili.

Juzi, haikuwa vita ya ngumi wala ya matumizi ya silaha za kudhuru, bali ya maneno au hoja za kisheria, lakini itakayoisha kwa wapiganaji wa pande zote kupeana mikono na kucheka kwa pamoja, kama ulivyo utamaduni wa mahakamani.

Pambano hilo lililosimamiwa na Jaji Sirillius Matupa, lilianza saa 4:16 asubuhi na kumalizika saa 2:44 usiku, wakati jaji alipolisitisha.

Lissu amewasilisha maombi ya kibali cha kufungua shauri kupinga kuvuliwa ubunge wake, lakini Serikali ikaweka vizuizi pingamizi la awali, kwa lengo la kumzuia asiuvuke kuelekea hatua nyingine ya kupigania ubunge wake.

Baada ya Jaji Matupa kuahirisha pambano hilo, kwa sasa kila upande unasubiri kutangazwa kwa matokeo hayo kesho saa 8:00 mchana.

Lissu amefungua maombi Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Dar es Salaam chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.

 

Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi la leo Jumapili Agosti 25, 2019