Saa 24 za hekaheka

Mtwara/Lindi. Taarifa za Kimbunga Kenneth katika mikoa ya Lindi na Mtwara jana, ziliibua taharuki kwa zaidi ya saa 24, idadi kubwa ya wananchi wakilala nje usiku baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kutoa tahadhari ya kuwapo kwa athari.

Mwandishi wa gazeti hili anayeripoti kutoka mkoani Mtwara alisimulia hali ya taharuki ilivyotokea katika maeneo mbalimbali na hatua zilizochukuliwa kabla ya kurejea kwa utulivu.

“Taarifa za kimbunga zilianza siku nne zilizopita kabla ya TMA kutoa taarifa juzi kwamba kitapita maeneo ya mkoa wa Lindi na Mtwara na watu wachukue tahadhari. Watu mbalimbali hapa Mtwara walikuwa wanapuuza taarifa hizo, walikuwa wanasema ni taarifa za kawaida zilizozoeleka,” alisema.

Lakini, baada ya mkuu wa mkoa huo kutoa taarifa ndipo watu wengi walianza kushtuka.”

Alisema, “usiku wa (jana) juzi nikiwa nyumbani lilipita gari likiwatangazia wakazi wa Shangani (Mtwara mjini) waondoke kwa muda, waende maeneo yaliyoandaliwa. Sikuwa na amani usiku huo hadi asubuhi (jana) nilipoanza kuona dalili za mvua.

“Asubuhi nikaenda Naliendele na baadaye nikarudi tena mjini kuangalia hali ikoje, nikapita mitaa ya Shangani, wananchi walionekana wakiendelea na shughuli zao za kawaida kama vile hakuna tahadhari yoyote iliyotolewa.”

Alisema, “niliwauliza baadhi ya wafanyabiashara wakasema hawana hofu yoyote, daladala zinafanya kazi kama kawaida, wakasema ni uvumi tu kama ilivyokuwa mwaka jana kuhusu mtoto aliyezaliwa bila meno na ilitakiwa watu waamke usiku wanywe uji.”

Mwandishi huyo alisema, “kwa hiyo wakapuuzia hivyo wakisema taarifa za TMA zilitakiwa kutokea ndani ya saa 24 lakini hadi jana kimbunga hakikutokea, nikaamua kurudi tena Naliendele.”

Alisema baada ya kufika huko alikutana na taarifa kuwa kimbunga hicho kingepita muda wowote huku picha za kutisha zikisambaa mitandaoni.

Kutoka mkoani Lindi, mashuhuda wa tukio hilo walizongumza na Mwananchi walisema kuanzia saa 12 asubuhi katika mitaa mbalimbali kulikuwa na idadi kubwa ya wananchi wakiwamo watoto na watu wazima waliokuwa barabarani, wengine ufukweni mwa bahari.

Pia, kulikuwa na idadi kubwa ya magari madogo yaliyokuwa yakitokea Mtwara kuelekea Dar es Salaam kuanzia saa moja asubuhi tofauti na ilivyo kawaida.

“Huwa naenda Mtwara kila wakati, hali ilikuwa tofauti kabisa na ilivyo kawaida, wakati narudi leo (jana) jioni eneo la Mikindani kulikuwa na watu wametanda baharini, kama wamepigwa na mshangao,” alisema Philip Ringo ambaye ni mfanyabiashara katika mikoa ya Kusini.

Nanyumbu

Baadhi ya wakazi wa Nanyumbu mkoani Mtwara walisema walisikia matangazo kupitia gari lililofungwa spika wakielezwa nini wafanye kuchukua tahadhali za kimbunga hicho.

Mmoja wa wananchi hao, Moses Joseph alisema gari hilo lilisaidia kufikisha taarifa haraka zaidi kwa wananchi hasa maeneo ya vijijini.

“Kuna maeneo hawasomi magazeti, hawana simu, redio wala TV sasa gari la matangazo limesaidia zaidi kwa sababu wengi wamepata ujumbe na kuchukua tahadhari,” alisema Joseph.

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Moses Machali aliwatuliza wananchi akiwataka watulie majumbani ikiwa maeneo wanayoishi ni salama.

Alisema ili kuepuka athali za kimbunga Keneth kilichotangazwa kuwa huenda kikayakumba maeneo hayo, wananchi hawapaswi kupata taharuki na kwamba, wametengeneza mfumo wa mawasiliano na Serikali za vijiji kupata taarifa zote muhimu iwapo kitatokea.

Machali alisema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na kimbunga hicho.

Alitaja makundi yaliyokuwa yakiendelea na kazi katika wilaya hiyo kuwa ni watumishi wa afya katika zahanati, vituo vya afya na hospitali.

“Pia vikosi vyote vya ulinzi na usalama kama polisi, wanajeshi wapo kazini kama kawaida na tumeandaa mtandao wa mawasiliano ya kupata taarifa popote likitokea jambo,” alisisitiza.

Alisema hali ya hewa tangu asubuhi ilikuwa ni tulivu na hakukuwa na madhara yoyote yaliyojitokeza.