Sababu Miss Tanzania kutopewa zawadi ya gari yabainishwa

Muktasari:

Mwandaaji wa shindano la Miss Tanzania amesema hawakuwa tayari kutaja zawadi ya mshindi iliyo nje ya uwezo wao halafu baadaye washindwe kumpatia na kuleta picha mbaya kwa jamii.

Dar es Salaam. Mwandaaji wa shindano la Miss Tanzania, Basila Mwanukuzi amesema kiasi cha Sh10 milioni walichokitoa kwa mshindi wa shindano hilo ndio ilikuwa uwezo wao.

Basila ameyasema hayo  katika fainali za shindano hilo, zilizomalizika usiku wa kuamkia leo Jumamosi Agosti 24,2019 jijini Dar es Salaam ambapo Silvia Sebastian kutoka mkoani Mwanza akiwakilisha Kanda ya Ziwa aliibuka mshindi.

Basila amesema hawakutaka kutaja zawadi kubwa ambayo baadaye ingewashinda kuitoa na kuibua maneno ndani ya jamii na kueleza kwamba kiasi walichokitoa ndio kilikuwa ndani ya uwezo wao.

Mbali ya uwezo pia amesema walitaka kubadilika katika kutoa zawadi ya gari na badala yake kumpa mshindi fedha ambayo ataenda kununua kile anachopenda mwenyewe.

"Hawa washiriki  katika shindano hili wengi wao ni wanafunzi, hivyo unapompa fedha inampa uwanja mpana wa nini akafanyie badala ya kumpa kitu," amesema Basila..

Hata hivyo, amesema kwa mwaka 2019 amekutana na baadhi ya changamoto ikiwemo kujitokeza kwa wadhamini wachache ukilinganisha na mwaka 2018.

Pamoja na changamoto hiyo, amesema yeye pamoja na kampuni yake ya 'The Look’ hawatarudi nyuma kwani walitarajia hayo kujitokea ukizingatia ndio mwaka wao wa pili kuyaandaa tangu yaliposimamishwa.

Kutokana na hilo amewashauri wadhamini kujitokeza, kwani wanapofanya hivyo inakuwa na faida kwa kila mmoja wao.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya mrembo aliyeshinda kuelekea mashindano ya   dunia ‘Miss World’,  amesema kwa mwaka 2019 wamemuandaa mapema na kubainisha suala la kuwa na shughuli ya kijamii ya kwenda kuiwasilisha, wameifanya kwa kila mshiriki aliyeshiriki.

"Hakuna aliyejua nani atakuwa mshindi usiku wa leo, hivyo tulichokifanya kila mshiriki alitakiwa kuandaa kazi yake ya kijamii ambayo kama ingetokea akashinda ndio atakayokwenda kuiwasilisha Miss World, hivyo kwa hilo hatuna shaka nalo," amesema Basila ambaye alikuwa Miss Tanzania mwaka 1998.

Pia, aliwasihi Watanzania kuonyesha umoja katika kufanikisha taji la Miss World linakuja Tanzania ikiwemo ushirikiano wao katika kupiga kura badala ya kazi hiyo kuonekana ni ya Basila peke yake na mrembo mwenyewe.