Sababu wakurugenzi mgodi wa Nyamahuna kukamatwa hizi hapa

Wednesday October 23 2019

By Rehema Matowo, Mwananchi [email protected]

Geita. Wakurugenzi watatu wa mgodi wa Nyamahuna unaomilikiwa na kampuni ya Eagle Brand Investment wamekamatwa na Polisi mkoani Geita kwa tuhuma za kuajiri raia wa kigeni wasio na vibali vya kufanya kazi Tanzania.

Akizungumza leo Jumatano Oktoba 23, 2019 kaimu kamanda wa polisi mkoani Geita, Dismus Kisusi amewataja wakurugenzi hao kuwa ni Andrew Bole, Dastan Moses na Msafiri wote wa Mkoa wa Geita.

Kukamatwa kwa wakurugenzi hao kumekuja baada ya kamati ya ulinzi ya mkoa kuwakamata raia 90 wa China wakifanya kazi katika mgodi huo bila kuwa na kibali.

Fundi sanifu wa migodi kutoka ofisi ya madini Geita ,Ramadhan Mcharo amesema raia hao wa kigeni wamekutwa wakifanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na wazawa  na kuitaka migodi yote kufuata sheria za kazi.

Ofisa kazi wa Mkoa wa  Geita, Mohamed Majaliwa  amesema raia hao wa kigeni hawana vyeti vinavyoonyesha taaluma zao na wengi wanafanya kazi za ulinzi na upishi jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Majaliwa amesema sheria ya kuratibu ajira za wageni namba 1 ya mwaka 2015 kifungu cha 9(a) ni kosa raia wa kigeni kufanya kazi nchini bila kuwa na kibali halali.

Advertisement

Amesema kuajiri raia wa kigeni bila kuwa na vibali halali vya ajira ni kosa kwa mujibu wa sheria na adhabu yake ni kulipa faini ya Sh10 milioni au kifungo cha miaka miwili au vyote kwa pamoja.

Hili ni tukio la pili la raia wa China kukamatwa katika mgodi huo wakifanya kazi bila kuwa na vibali.

Februari 16, 2016 raia 16 wa China walikamatwa mkoani Geita kwa tuhuma za kukiuka taratibu za uhamiaji na kufanya kazi kinyume cha sheria.

Advertisement