Sababu wananchi Busokelo kukosa maji wiki tatu yatajwa

Muktasari:

Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya (Mbeya -Uwasa) imepata hasara ya zaidi ya Sh15 milioni baada ya wananchi wasiojulikana kufukua mabomba ya maji.

 

Mbeya. Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya (Mbeya -Uwasa) imepata hasara ya zaidi ya Sh15 milioni baada ya wananchi wasiojulikana kufukua mabomba ya maji.

Eneo lililoathirika ni makao makuu ya Ruangwa halmashauri ya Wilaya ya Busokelo.

Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka hiyo,  Ndele Mengo ameieleza Mwananchi Digital leo Jumatatu Oktoba 20, 2020 kwamba uharibifu huo umesababisha hadi leo jioni kaya 20,000 kukosa huduma ya maji  kwa wiki tatu.

Mengo amesema kuwa mradi huo ambao Serikali imetumia zaidi ya Sh1.6 bilioni umekamilika kwa asilimia 90 na wananchi tayari walikuwa wameanza kunufaika nao lakini watu kwa kukosa uadilifu wameharibu.

"Ni jambo la kushangaza mradi huu mpya umeanza kutumika mwezi Julai mwaka huu wananchi wamefanya uharibifu katika eneo ambalo mabomba yanatoa maji kwenye chanzo kupeleka kwenye tanki ambalo linasambaza maji kwa wateja," amesema.

Aidha amesema kufuatia changamoto hiyo Mamlaka imelazimika kutumia mapato ya ndani kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na mabomba na kufanya matengenezo ili kurejesha huduma maji safi kama kawaida.