Sadc: Tanzania imevuka vigezo ukuaji wa uchumi

katibu mtendaji wa Sadc, Dk Stegomena Tax

Muktasari:

Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) imesema licha ya kwamba nchi wanachama wa jumuiya hiyo zinajitahidi kukua kiuchumi lakini Tanzania ni mfano wa kuigwa kutokana na kuvuka vigezo na kufikia ukuaji wa uchumi wa asilimia 7.

Dar es Salaam. Tanzania imetajwa kuvuka vigezo vya ukuaji uchumi kati ya nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Imetajwa kuwa ni nchi ambayo imefanikiwa kukua kiuchumi kwa muda mfupi.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Agosti 17, 2019 na katibu mtendaji wa Sadc, Dk Stegomena Tax  wakati akifungua mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo unaofanyika leo na kesho katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC)

Dk Tax amesema uhimilivu wa uchumi ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo kwa nchi wanachama na kuzihamasisha nchi nyingine kukua kiuchumi.

"Nchi zilizokidhi vigezo katika nchi wanachama ni nyingi zinafanya vizuri na Tanzania ni nchi pekee iliyofikia kigezo cha asilimia 7 katika ukuaji uchumi. Huu ni mfano wa kuigwa,” amesema Dk Tax.