Sadc yajidhatiti kufikia soko la pamoja kupitia sekta ya miundombinu na uchukuzi

Muktasari:

  • Wakati mkutano wa Baraza la Mawaziri Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) ukizinduliwa leo kwa kikao cha makatibu wakuu, mkazo zaidi umeendelea kuwekwa katika kuhakikisha miundombinu inaboreshwa ili kufanikisha mkakati wa soko la pamoja.

Dar es Salaam. Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc)  imesema kwa kuwa malengo ya pamoja kwa nchi 16 wanachama ni kuwa na soko la pamoja ifikapo 2050, uwekezaji katika miundombinu hauepukiki.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Septemba 16, 2019 na Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma katika Sekretarieti ya Sadc, Mapolao Mokoena wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Sadc.

Mokoena amesema bila kuwa na miundombinu ya uhakika ni ndoto kwa nchi hizo kufanikiwa katika soko la pamoja.

“Kuna ulazima wa kutoa kipaumbele katika kuimarisha miundombinu ya uchukuzi ili kutoa fursa za kibiashara kwa wakazi ndani ya jumuia ya nchi za Sadc, bila hivyo hatutaweza kufikia malengo mengine makuu ikiwamo kuendeleza viwanda. Malengo yetu kufikia mwaka 2050 tuwe na soko la pamoja katika hili tunaweza kuzitumia nchi zilizoanza kufanikiwa kama Tanzania katika uwekezaji wa miundombinu,” amesema.

Mkutano huo wa siku tano wa baraza la mawaziri umezinduliwa leo  na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe ukitanguliwa na vikao vya makatibu wakuu kwa siku tatu na baadaye kumaliziwa na mawaziri kutoka nchi 16 wanachama.

Makatibu wakuu wanaoshughulikia wizara za Tehama, Habari, Uchukuzi na Hali ya hewa kutoka Sadc wamekubaliana kutoa kipaumbele katika miundombinu ya uchukuzi na mawasiliano ili kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Majadiliano na makubaliano hayo ni utaratibu wa kawaida kwa Sadc katika kuelekea kilele cha mkutano wa mawaziri wanaoshughulikia sekta hizo zinazotajwa kuwa muhimili mkubwa katika kufikia azma ya maendeleo katika jumuia hiyo iliyodumu kwa zaidi ya miongo miwili na nusu.