Samia aongoza ujumbe wa Serikali kuaga mwili wa Balozi Kaduma

Muktasari:

Makamu wa Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan ameongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa Balozi Ibrahim Kaduma.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan ameongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa Balozi Ibrahim Kaduma.

Ibada ya pili kuaga mwili wa Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje nchini Tanzania itaanza leo Jumanne Septemba 3, 2019 saa 7 mchana katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)  Makongo Juu.

Mbali na Samia, marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete pamoja na katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally watashiriki ibada hiyo.

Akimzungumzia Kaduma, Dk Bashiru amesema kiongozi huyo ataendelea kuishi moyoni mwake kwa sababu ameacha maandishi ya alichokiamini.

"Amesisitiza sana maana ya maadili kwa viongozi wa umma na hata kwenye chama, aliishi kile alichoamini na tunaobaki tunapaswa kumuenzi kwa vitendo," amesema Dk Bashiru.

Mmoja waliowahi kusoma kitabu cha Balozi Kaduma cha 'Maadili ya Taifa na Hatma ya Tanzania', Sinza Godigodi amesema Balozi Kaduma aliamini elimu peke yake haitoshi kama huna maadili.

Kinachoendelea sasa ni kuaga mwili wakati ibada ikisubiriwa kuanza.

Mwili wa Balozi Kaduma unatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda nyumbani kwake Kibena Njombe kwa ajili ya mazishi.