Schumacher aenda kutibiwa jijini Paris

Tuesday September 10 2019

Schumacher , jijini Paris,Georges-Pompidou,mwananchi habari,

 

Michael Schumacher, ambaye ametwaa ubingwa wa dunia wa mbio za magari aina ya langalanga mara saba, yuko hospitali ya Georges-Pompidou jijini Paris kupata matibabu ya seli, kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Le Parisien.

Idara ya uhusiano ya hospitali hiyo haikukanusha wala kuthibitisha taarifa za kuwepo kwa bingwa huyo ilipoulizwa na AFP, ikieleza kuwa sera za faragha za hospitali zinawazuia.

Lakini kwa mujibu wa Le Parisien, dereva huyo Mjerumani mwenye umri wa miaka 50, anatibiwa kitengo cha moyo na daktari wa upasuaji, Philippe Menasche, ambaye anaelezewas kama bingwa wa upasuaji wa masuala ya seli wakati moyo unaposhindwa kufanya kazi.

"Matibabu yataanza Jumanne asubuhi na ataondoka hospitalini Jumatano," limeandika gazeti la Le Parisien, ambalo pia limedai nyota huyo wa timu ya Ferrari ameshatibiwa hospitalini hapo mara mbili.

Dereva huyo maarufu wa magari ya langalanga alijeruhiwa katika ajali iliyotokea wakati akishiriki mchezo wa kutereza juu ya barafu baada ya kuanguka wakati kofia yake ngumu ikiwa imevuka Desemba, 2013 na habari chache kuhusu hali yake zimekuwa zikitolewa hadharani tangu wakati huo.

Alipoteza fahamu kwa miezi sita baada ya kudondoka na kuhamishwa kutoka hospitali ya Grenoble kwenda Lausanne kabla ya kurudishwa nyumbani Septemba 2014 ambako anapata matibabu binafsi.

Advertisement

Marafiki wake wa zamani wanasema hawezi kutembea na hazungumzi vizuri.

Schumacher alishinda ubingwa wa kwanza wa dunia miaka 25 iliyopita na alitwaa ubingwa wa mashindano makubwa ya Grand Prix kwa mara ya kwanza mwaka 1992. Mara zote ameshinda akiwa na timu za Benetton na Ferrari, ambayo aliitumikia wakati aliposhinda mataji la mwisho.

Aliamua kuachana na kustaafu mwaka 2010 na kuitumikia timu ya Mercedes kwa miaka mitatu.


Advertisement