Selasini aeleza Lissu alivyopigwa risasi Dodoma -VIDEO

TUNDU LISSU APIGWA RISASI, HALI YAKE MBAYA

Muktasari:

  • Mbunge Joseph  Selasini amesema Lissu alianza kufuatiliwa tangu alipotoka bungeni

Dodoma. Mbunge wa Rombo, Joseph  Selasini ameeleza jinsi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alivyopigwa risasi nyumbani kwake mjini Dodoma.

Selasini amesema kuwa maelezo aliyopata ni kuwa alikuwa akifuatiliwa na  gari tangu anatoka bungeni na dereva wake alilishtukia.                       

Amesema kuwa alivyoona wanamfutilia alipofika nyumbani, dereva alimsihi Lissu asishuke ndani ya gari.                        

"Hao watu walipoona hawashuki walijifanya kuna kitu wanaangalia walivyoona kuna utulivu walisogeza gari lao ambalo ni tinted na kuanza kurusha risasi upande wa Lissu." amesema                       

Selasini amesema, “Risasi zilimpata mguuni, mkononi na tumboni lakini daktari anasema anaendelea vizuri."

Lissu amepigwa risasi leo Alhamisi  na kupelekwa chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, wabunge na viongozi wengine wa ulinzi wa Bunge wamefika katika hospitali hiyo kujua kinachoendelea.

Baadhi ya ndugu na wagonjwa wamefurika katika chumba cha upasuaji cha hospitali ya mkoa wakitafakari huku wengine wakilia.