Seneta Bernie Sanders asitisha kampeni Marekani

Muktasari:

Seneta Bernie Sanders ametangaza kusitisha kampeni za kuwania tiketi ya kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic.

Washington. Seneta Bernie Sanders ametangaza kusitisha kampeni za kuwania tiketi ya kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic.

Kusitisha kampeni kwa Sanders (78) kunafungua njia kwa makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Joe Biden ambaye aliyekuwa anachuana naye ndani ya chama hicho.

Seneta Sanders amesitisha kampeni jana Jumatano Aprili 8, 2020 na kuwaeleza  wafuasi wake kuwa haoni kuwa atapata kura za kutosha kuteuliwa kuwa mgombea wa chama hicho.

Sanders ambaye alionekana kuwa na mvuto kwa wapiga kura vijana alikuwa anachuana na Biden ambaye ni makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo.

Wagombea wengine akiwamo Amy Klobuchar na Pete Buttigieg walitangaza kusitisha kampeni zao na kumuunga mkono Biden.

Mwingine aliyesitisha kampeni ni Beto O'Rourke aliyetangaza kumuunga mkono Biden.

Hivi karibuni Sanders amekuwa akifanya kampeni kupitia mitandao ya kijamii kutokana na mlipuko wa virusi vya corona

Biden (77) sasa anasubiri kutawazwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Democratic mwezi Agosti ili kuchuana na Rais Donald Trump ambaye atatetea kiti hicho kwenye uchaguzi mkuu Novemba, 2020.