Serikali Tanzania yapiga ‘stop’ twisheni, yabainisha mbadala

Muktasari:

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania imesisitiza kuwa hakuna mwalimu anaruhusiwa kuendesha madarasa ya ziada ‘twisheni’ katika kipindi ambacho wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo wakiwa majumbani kwa siku 30 kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona kuendelea kusambaa nchi mbalimbali duniani ikiwamo Tanzania.

Dar es Salaam. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania imesisitiza hakuna mwalimu anaruhusiwa kuendesha madarasa ya ziada na badala yake wazazi na walezi wawasisitize watoto wao kujisomea wenyewe nyumbani.

Uamuzi huo unalenga kupungua uwezekano wa kusambaa virusi vya corona (Covid-19) kama ambavyo Serikali ya Tanzania Machi 17, 2020 iliamua kufunga shule na vyuo vyote nchini kwa siku 30.

Akizungumza na Mwananchi Naibu waziri wa Elimu William Ole Nasha alisema kwa kuwa hadi sasa mwelekeo wa ugonjwa huo haujaeleweka ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha wanasoma na kuyaelewa yale waliyofundishwa kabla ya shule kufungwa.

Alisema watoto ni kundi ambalo linaweza kuambukizwa ugonjwa huo kwa urahisi kutokana na kushindwa kuchukua tahadhari ndiyo sababu imezuiwa

mikusanyiko yote inayohusu kundi hilo.

“Tumepiga marufuku masomo ya ziada kwa kuwa ni yanachangia mkusanyiko, unajua watoto ni vigumu sana kwao kuchukua tahadhari, ukiwaweka pamoja

inaweza kuwa chanzo cha kusambaa  maabukizi,” alisema Ole Nasha.

Alisema kwa watoto ambao hawawezi kuvifikia vifaa ya Tehama wanatakiwa kusoma  na kujifunza kwa kina yaliyomo kwenye daftari  na vitabu vyao.

“Kuna wazazi wanaweza kuwasaidia watoto wao kusoma kwa njia ya Tehama wasisite kufanya hivyo kupitia programu mbalimbali. Katika hili Taasisi ya Elimu Tanzania ina maktaba mtandao, mtoto anaweza kuingia huko na kukutana na vitabu vya kila aina,” alisema