Ukimya wa Serikali madai tume huru ya uchaguzi unavyoibua mijadala

Tangu kuibuliwa kwa kilio cha kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi nchini, Serikali imekuwa kimya.

Hatua hiyo imesabababisha viongozi wa vyama vya upinzani kuendelea kutoa kilio hicho kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.

Ingawa Rais John Magufuli ameshasema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa huru na wa haki, madai hayo yameendelea kutolewa na wanasiasa ambao wengi wao wanasema hawawezi kuamini maneno matupu bila kuwapo kwa vitendo vinavyoendana na kauli hiyo.

Wanasema kauli hiyo inapaswa kurandana na vitendo kuelekea uchaguzi ikiwamo kufanyiwa kazi madai ya muda mrefu ya kasoro zinazojitokeza katika uchaguzi.

Juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliendeleza kilio hicho katika msiba wa Elias Mwingira, baba wa kiongozi wa kanisa la Efatha, Mtume na Nabii Josephat Mwingira.

Mbowe alisema kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, kwa hali ilivyo kuna kila aina ya kiashiria cha kutokea machafuko ya kisiasa kama viongozi hawatazika viburi vya kiitikadi na kusimama pamoja.

Kilio hicho hakikuanza hapo, kwani hivi karibuni, Mbowe aliviambia vyombo vya habari kuwa Januari 29, 2020 alimwandikia barua Rais John Magufuli kuomba Serikali kufanya mabadiliko ya sheria yakayowezesha kuundwa kwa tume huru kabla ya Oktoba.

Kabla ya hatua hiyo, Desemba 9 mwaka jana jijini Mwanza katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika jijini Mwanza, Mbowe aliomba kuwapo kwa maridhiano ya kitaifa mbele ya Rais Magufuli.

“…Rais una nafasi ya kipekee kuweka historia ya maridhiano katika taifa letu kwani kuna wengine wanalalamika wanaumia. Rais tumia nafasi hii ukaliweke taifa katika hali ya utengamano,” alisema Mbowe.

Pia Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulitoa taarifa ukitaka kuharakishwa kwa uanzishwaji wa tume huru ya uchaguzi na kuteuliwa mapema kwa waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa wa kuaminika watakaofuatilia uchaguzi kwa kipindi kirefu na kifupi.

Pamoja na hayo, kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema msimamo wa chama hicho katika chaguzi zijazo ni kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi, ili uchaguzi wa 2020 usiwe na dosari kama zilizotokea katika chaguzi zilizopita.

Alisema bia kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi pasiwe na uchaguzi wowote nchini na kuwataka viongozi wa kitaifa wa vyama wametoe tamko la pamoja kutaka tume huru ya uchaguzi.

Ukiacha kilio hicho kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini, mjadala wa jambo hilo pia upo katika mitandao ya kijamii.

Mtu aliyejitambulisha kwa jina la Tonny Adamms kupitia ukurasa wa Twitter alisema: CCM iko tayari kushindana, sawa, lakini kushindana uchaguzi ukisimamiwa na tume gani ya uchaguzi? Kwanini mnaiogopa Tume Huru ya Uchaguzi?

“Kama hamuogopi iundwe tume huru ya uchaguzi mara moja, nitawapongezeni sana, kitakachobaki sasa ni kusikiliza hoja za kila chama”.

Naye mtu aliyejitambusha kama John Mazanda alisema: “Hivi akili zenu zinawaonyesha kwamba tuliyonayo ni tume huru?? Mnaogopa nini kuruhusu tume huru isiyoteuliwa na mwenyekiti wa chama? Is this need a degree to understand?”

Kwa upande wake Sha Mwenda@mwenda_sha anasema: “Tume huru ya uchaguzi ndio mpango mzima”.

Kilio cha kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi nchini kimekuwepo kwa muda mrefu sasa na viongozi hao wanaendeea kukitoa kwa kuwa bado Serikali haijatoa kauli ya kulishughulikia jambo hilo.

Tangu kuanza kutolewa kwa kilio hicho, Serikali zimekuwa kimya, huku chaguzi zikiendelea kufanyika na kuja nyingine.

Ukimya wa Serikali katika jambo hili ni hatari kwa mustakabali wa taifa, kwani unaweza kukwamisha michakato ya uchaguzi kutokana na wananchi kukata tamaa ya kufanyika kwa uchaguzi ulio huru na wa haki.

Yaliyotokea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka jana na kusababisha baadhi ya vyama vya siasa kususia uchaguzi, si vema yakajirudia katika uchaguzi mkuu mwaka huu, kwani yataendelea kufifisha demokrasia nchini.

Madai ya kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi yana takriban miaka 30 sasa na yamekuwa yakiibuka na kutoweka kulingana na nyakati, lakini zaidi nyakati za uchaguzi.

Madai haya yalianza mwaka 1991 baada ya Serikali ya awamu ya pili, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi alipounda tume ya kukusanya maoni kuhusu mfumo wa vyama vya siasa iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali. Miongoni mwa mapendelezo yaliyotolewa ni kuwpao kwa tume huru ya uchaguzi.

Baada ya tume ya Nyalali, zilifuata tume nyingine ya Jaji Robert Kisanga na ya Jaji Joseph Warioba ambazo kwa nyakati tofauti zilikuja na mapendekezo ya kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi.

Hata hivyo, hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu swali la Mbowe bungeni alisema tume iliyopo ni huru.

Majaliwa alisema suala hilo lilishatolewa majibu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama na yeye amerudia.

“Tume hii imeundwa kwa mujibu wa Katiba, na kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi kipengele 78, 74 na kipengele kidogo cha 7, 11 na 12 kinaeleza kwamba hiki ni chombo huru.

“Kimeelezwa pia kwenye Katiba pale kinaundwaje na chombo hiki hakipaswi kuingiliwa na chombo chochote, iwe Rais wa nchi, iwe chama chochote cha kisiasa au mamlaka nyingine yoyote ile haipaswi kuingilia.

“Kama ni chombo huru kwa mujibu wa Katiba, ndio tume huru! Sasa kunaweza kuwa kuna tofauti ya neno huru hili tunataka itambulike vipi, chombo kipo, kinajitegemea na kinafanya kazi yake bila kuingiliwa na mtu yeyote kwa mujibu wa Katiba yetu ya mwaka 1977,” alisema Majaliwa.

Hata hivyo, Mbowe alisema majibu ya Waziri Mkuu ni mepesi na kuna siku watakuja kujuta kutokana na majibu hayo.

Naye Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alinukuliwa hivi karibuni katika ukurasa wa Twitter wa CCM akisema,” Wapo wanaolilia tume huru kupata ushindi. Tume huru haipigi kura bali inasimamia uchaguzi. Chama kisicho na wapigakura kisitegemee tume iwape ushindi. CCM imetafuta wapigakura kwa kutoa elimu bure, afya, maji na barabara, sasa wao waseme wapigakura wamewapataje”.

Kauli hiyo ya Dk Bashiru iliibua mjadala kwa badhi ya wachangiaji ambao walihoji utekeleaji wa maeneo unaofanywa na CCM na uhusiano wake na Tume ya Uchaguzi.

Mmoja wa wachangiaji hao aliyefahamika kwa jina la Armoured @EngNyahucho alisema: “Suala si ushindi, na kama mnaamini mnapendwa basi kubalieni tupate Tume Huru, woga wa nini na huku mna uhakika wa ushindi”.