Serikali tatu ilivyomng’oa Aboud Jumbe madarakani

Safari ya miaka mitano ya Aboud Jumbe aliyoianza Oktoba 30, 1980 baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar iligota Januari 30, mwaka 1984.

Aliapishwa baada ya kuibuka mshindi kwa kupata kura 174,672 za ndiyo kati ya kura 186,517 zilizopigwa katika uchaguzi huo uliofanyika Jumapili Oktoba 26,1980, sawa na asilimia 93.65 ya kura zote.

Kura za hapana zilikuwa 5,508, huku kura 6,337 zikiharibika. Jumla ya watu 199,946 walijiandikisha kupiga kura.

Uchaguzi huo wa urais mwaka 1980 ulikuwa wa kwanza Zanzibar kufanyika tangu Mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Kabla ya uchaguzi huo, Jumbe, aliyekuwa na umri wa miaka 60, alianza kuiongoza Zanzibar Aprili 1972 baada ya kifo cha Abeid Amani Karume.

Jumbe hakumaliza miaka mitano kama yalivyo matakwa ya kikatiba. Alitimuliwa ukiwa umesalia mwaka mmoja na nafasi yake ikachukuliwa na Ali Hassan Mwinyi.

Ulikuwa uamuzi uliochukuliwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM chini ya mwenyekiti wake, Mwalimu Julius Nyerere ili kuzima fukuto la haja ya Muungano wa Serikali tatu ambalo Jumbe alikuwa akilipigania.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala na mwandishi wa habari mkongwe nchini, Allan Lawa wanatoa simulizi ya kile kilichojiri kabla na baada ya uchaguzi huo na kuondolewa kwa Jumbe madarakani kuwa ni mtazamo na msimamo wake wa kudai Zanzibar huru.

Profesa Mpangala anasema baada ya mapinduzi, Zanzibar haikuwa na Bunge wala Katiba na kulikuwapo na Baraza la Mapinduzi pekee.

Anasema mwaka 1979, Jumbe aliamua kutengeneza Katiba ya Zanzibar.

“Katika katiba ile ikapendekezwa kuwe na Baraza la Wawakilishi na kuwe na uchaguzi ya kila miaka mitano na Rais achaguliwe na wananchi,” anasema Profesa Mpangala.

“Jumbe alikuwa anajenga misingi ya kidemokrasia kutoka ile ya mapinduzi.”

Mhadhiri huyo anasema kati ya mwaka 1983 na 1984 kulitokea vuguvugu jingine la kuitaka Zanzibar kuwa huru, yaani muungano wa Serikali tatu na Jumbe alikuwa anaupigania.

“Sasa lile vuguvugu alilisimamia Jumbe na mwaka 1984 kikatokea kitu kilichoitwa uchafuzi wa hali ya kisiasa Zanzibar ya kudai serikali tatu ambayo ilimgharimu Jumbe kwa kuwa taarifa zilipofika kwa Rais wa wakati ule Mwalimu Nyerere aliyekuwa mwenyekiti wa CCM, aliitisha kikao cha Halmashauri Kuu Dodoma,” anasema.

Profesa Mpangala anasema katika kikao hicho, Jumbe alifukuzwa na nafasi yake ikachukuliwa na Ali Hassan Mwinyi aliyeongoza kwa mwaka mmoja huku Waziri Kiongozi akiwa, Maalim Seif Sharif Hamad.

“Mwinyi akawa Rais wa mwaka mmoja na Maalim Seif akawa waziri kiongozi na waliiongoza vizuri sana Zanzibar katika nyanja mbalimbali na kufufua uchumi,” anasema Profesa huyo.

“Ile ilimpa sifa sana, na Mwalimu Nyerere alipomaliza muda wake, Mwinyi akapitishwa na CCM kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku Zanzibar akiteuliwa Abdul Wakili,” anasema.

Anasema mwaka 1988 kulitokea vurugu ambazo anasema hazikumbuki vizuri kati ya Wakili na Maalim Seif hali iliyomfanya Maalim Seif kuondoka.

Jumbe alikuwa maarufu

Mwandishi mkongwe nchini, Allan Lawa anasema Jumbe alikuwa maarufu sana kwa sababu ni mmoja wa walioshiriki mapinduzi na maarufu chini ya mfumo wa chama kimoja.

Anasema anakumbuka Jumbe akiwa rais, waziri kiongozi alikuwa Maalim Seif ambaye naye alikuwa kijana maarufu aliyependa sana elimu na aliisimamia vyema.

Lawa anasema uchaguzi wa chama kimoja haukuwa na msisimko ikilinganisha na ule wa wawakilishi.

“Ilikuwa amshaamsha ya aina yake na kila mmoja alimpigania Rais kuhakikisha anakwenda kumpigia kura huku mchuano ukibaki kwa nafasi za uwakilishi,” anasema

Lawa, aliyewahi kufanya kazi Baraza la Habari Tanzania (MCT), anasema “hata katika vitabu alivyoandika, JUmbe alikuwa anaamini katika Muungano ila wa Serikali tatu. Alisema Zanzibar inahitaji uhuru zaidi kuliko kuvishwa muungano pasina mamlaka”.

Mwananchi ilipotaka kujua sababu za misimamo ya Jumbe, kutojulikana mapema hadi CCM ikampitisha kugombea urais, Lawa anasema: “Kuna msemo unasema nipe cheo uone tabia yangu.”

“Mzee Jumbe akiwa rais, mimi nilikuwa kazini,” anasema Lawa.

“Uchaguzi wa kwanza kupiga kura ilikuwa mwaka 1975 na mwaka 1980 huenda Jumbe alijificha kwa kile alichoamini cha serikali tatu, lakini baada ya kupewa urais alianza kusema kile alichokuwa anachokifikiria.”

Kuhusu kile alichokuwa anakipigania na maoni ya Wazanzibari waliyoyatoa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya mfumo huo wa muungano, Lawa anasema hilo lipo kwa wananchi hao.

“Wazanzibar na Zanzibar yao, ukiongea nao katika korido, wanataka serikali tatu,” alisema.

“Kuna makundi kule Zanzibar ambayo ili wakupokee ukiwa unatoka Tanzania Bara, sema unatoka Tanganyika, lakini ukisema unatoka Tanzania Bara watakuuliza visiwani ni wapi,” anasema Lawa.

“Baadhi ya makundi ya Zanzibar na viongozi walitoa maoni yao mbele ya kamati ya mabadiliko ya katiba wakitaka serikali tatu, lakini hawawezi kuja hadharani na kusema.”

Anachokumbuka Maalim Seif

Maalim Seif, ambaye sasa ni mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, anasema baada ya mapinduzi, katiba ya uhuru ya mwaka 1963 ilisimamishwa na Zanzibar ikawa inaendeshwa kwa amri za rais (decree).

“Ingawa zinaitwa amri za rais, lakini kabla ya kutangazwa amri yoyote ile, decree hiyo ilijadiliwa katika Baraza la Mapinduzi. Kipindi hicho (1964-1980) kulikuwa hakuna Bunge/Baraza la Wawakilishi! Baraza la Mapinduzi lilikuwa chombo cha uendeshaji nchi na pia chombo cha kutunga sheria,” anasema

Anasema mwaka 1979 akiwa waziri wa elimu, alikuwa mjumbe wa baraza la wawakilishi ambalo lilikaa na kutunga katiba na rasimu yake iliandaliwa na rais wa Zanzibar wa wakati huo, Jumbe, kwa kushirikiana na mwanasheria mkuu wa Serikali na wanasheria wengine.

Iliwasilishwa katika Bunge la Katiba na baada ya majadiliano ya karibu wiki nzima, rasimu ikapitishwa na kuwa katiba ya Zanzibar ya 1979.

Ilikuwa ni katiba ya kwanza

Maalim Seif anasema katiba hiyo ndiyo iliyoleta mfumo wa kuwa na vyombo vitatu vya serikali, kila kimoja kikiwa huru.

“Vyombo hivyo ni chombo cha kuendesha serikali, ambacho kwa Zanzibar kilibaki na jina la Baraza la Mapinduzi. Chombo cha pili ni cha kutunga sheria ambacho kiliitwa Baraza la Wawakilishi. Na chombo cha tatu kilikuwa cha kutoa haki , yaani mahakama,” anasema.

Anasema katiba ya 1979 ilianza kutumika rasmi Januari 12, 1980 ambayo Katiba hiyo ilianzisha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Pia, Katiba hiyo ilieleza Rais atachaguliwa kwa kura za wananchi.

“Katiba hiyo ilieleza kutakuwa na wagombea wawili tu wa Rais ambao wangeteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM,” anasema.

Maalim Seif aliyewahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar anasema katika uchaguzi huo wa 1980 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa iliwapendekeza wagombea wawili kugombea nafasi ya Rais wa Zanzibar ambao ni Aboud Jumbe na Idris Abdul Wakil ambao wote kwa sasa ni marehemu.

“Majina hayo yalifikishwa mbele ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Katika kikao cha Halmashauri Kuu kilichoitishwa kushughulikia uteuzi wa wagombea urais Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar, Mzee Idris Abdu Wakil aliomba kuondosha jina lake na Mzee Aboud Jumbe alipitishwa kwa asilimia 100 ya wajumbe wa Halmashauri Kuu,” anasema.

“Hivyo, Tume ya Uchaguzi ilitayarisha karatasi za kura ambazo upande mmoja ilikuwa na picha na jina la mgombea na upande wa pili ni picha inayofanana na ukuta. Kwa ufupi wapigakura walitakiwa kupiga kura ya ‘ndio’ au ‘hapana.”

Anasema kabla ya uchaguzi huo kulikuwa na kipindi cha kampeni ambayo ilisimamiwa na CCM.

Maalim Seif anasema uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLM) ulikuwa wa aina yake. Wakati huo katika kila Mkoa kulikuwa na Kamati ya Mapinduzi na hivyohivyo kwa kila wilaya.

Anasema wajumbe wa kamati ya mapinduzi wa mkoa walichagua wajumbe wawili wa BLW.

“Mimi nilichaguliwa na wajumbe wa kamati ya mapinduzi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba. Kwa mikoa mitano ya Zanzibar walipatikana wajumbe wa BLW 10.”

“Kila wilaya nayo ilichagua wajumbe wawili. Kwa wilaya 10 walipatikana wajumbe wa BLW 20. Jumla ni 30. Wajumbe wengine wote wa BLM ambao walikuwa 32. Rais aliteua wajumbe 10, ukimuongeza Mwanasheria mkuu wa Serikali ulipata jumla ya Wajumbe wa BLW 73,” anasema.