Serikali ya Tanzania, Barrick waunda kampuni ya Twiga kusimamia madini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Profesa Palamagamba Kabudi.

Muktasari:

  • Serikali imetangaza kuundwa kwa kampuni mpya ijulikanayo kwa jina la Twiga Minerals itakayokuwa na majukumu ya kuangalia uendeshaji wa migodi mitatu ya Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu.

Dar es Salaam. Baada ya mgogoro uliodumu tangu mwaka 2017, Kampuni ya Barrick na Serikali zimeunda kampuni ya Twiga itakayosimamia migodi mitatu iliyokuwa chini ya kampuni ya Acacia.

Kwenye kampuni hiyo mpya, Barrick itamiliki asilimia 84 ya hisa zote huku Serikali ikiwa na asilimia 16. Utaratibu huo ni utekelezaji wa sheria mpya ya madini iliyopitishwa mwaka 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Profesa Palamagamba Kabudi amesema ‘sasa amezaliwa mtoto mpya baada ya Barrick kukubali kumuua mtoto wake, Acacia.’

Mgogoro kati ya Serikali na kampuni ya Acacia iliyokuwa inasimamia migodi ya Buzwagi, North Mara na Bulanhulu ulianza mwaka 2017 na Rais John Magufuli akaunda tume ya kuchunguza mwenendo wa biashara ya madini.

Tume hiyo ilibaini ukiukwaji wa sheria, utaratibu na kanuni zilizopo hivyo kuikosesha Serikali mapato inayostahili. Kutokana na hilo, Serikali iliipiga faini ya Dola 190 bilioni jambo lililosababisha kuanza kwa mzungumzo baina ya pande hizo mbili.

Kwenye mazungumzo hayo, Acacia ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick iliwekwa pembeni na majadiliano yakafanywa na Barrick…mwisho wa siku, Acacia imefutwa sokoni na badala yake, Twiga itachukua nafasi yake.

“Twiga Minerals Company Limited itakuwa na makao makuu yake jijini Mwanza. Kampuni hii imeundwa baada ya kufutwa kwa Acacia iliyokuwa na makao makuu yake jijini London,” alisema Kabudi.