Serikali ya Tanzania kuajiri watumishi wapya 44,811

Muktasari:

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Tanzania, George Mkuchika amesema katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali inatarajia kuajiri watumishi wapya 44,811.

Dodoma. Serikali ya Tanzania inatarajia kuajiri watumishi wapya 44,811 katika mwaka wa fedha 2020/2021.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 15, 2020 wakati akiwasilisha bajeti yake kwa mwaka huo wa fedha.

Ametaja ajira hizo mpya kuwa ni kada ya elimu (13,529), afya (10,467), kilimo, mifugo na uvuvi (2,145) Jeshi la Polisi (2,725), magereza (685), Jeshi la zimamoto (501), uhamiaji (495) na hospitali za mashirika ya kidini na hiyari (1,262).

Aidha, amesema Serikali inatarajia kuajiri watumishi 13,002 wa kada nyingine zikiwamo za wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma nchini.

Mkuchika amesema pia Serikali itawapandisha vyeo watumishi 222,290 wa kada mbalimbali kulingana na maelekezo yatakayotolewa.