Serikali ya Tanzania kuanzisha kliniki ya ufugaji

Saturday March 07 2020
pic mifugo

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo, Elisante Ole Gabriel akizungumza na vyama vya wafugaji kuku na Nguruwe

Dar es Salaam. Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo nchini Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel amesema wanatarajia kuanzisha kliniki za kutoa ushauri wa ufugaji katika kila halmashauri ili kuongeza thamani ya ngozi inayozalishwa.

Profesa Gabriel ameyasema hayo leo Jumamosi Machi 7, 2020 jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na vyama vya wafugaji kuku na nguruwe pamoja na wadau wa ngozi uliolenga kupokea changamoto ili zitafutiwe ufumbuzi.

Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo Ole Gabriel amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanunuzi kuwa kuna baadhi ya ngozi haikidhi viwango vya ubora unaotakiwa katika uzalishaji bidhaa jambo ambalo limekuwa likiikosesha serikali mapato.

“Sasa ili kukabiliana na suala hili, mimi nikishirikiana na mwenzangu kutoka Tamisemi tuko katika hatua mbalimbali ili kuhakikisha kila halmashauri inakuwa na kliniki ya mifugo,” amesema

Amesema katika sehemu hiyo mfugaji ataweza kupata elimu ya namna ya kutunza mifugo yake huku akitolea mfano wa ng’ombe kuanzia akiwa na mimba, baada ya kuzaa na namna ya kumtunza hadi anakuwa mkubwa ili aweze kuleta faida inayokusudiwa na wafugaji.

“Suala hili litaenda mbali zaidi na kufikia katika hatua za uchinjaji ambapo visu maalumu vitasambazwa katika maeneo na elimu maalumu ya uchunaji inayozingatia viwango itatolewa,” amesema

Advertisement

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Wadau wa ngozi Tanzania, Adam Ngamilo ameonyesha kufurahishwa na uamuzi wa serikali huku akibainisha kuwa utawasaidia katika kuboresha mnyororo wa thamani za bidhaa.

“Suala hili lilikuwa ni changamoto sana kwetu hasa sisi viongozi tunaomaliza muda tunaamini watakaoingia wataitumia ipasavyo,” amesema Ngamilo

Kwa upande wa wafugaji wa kuku wameiomba Serikali kuwasaidia kupata mitaji ili waweze kufanikisha malengo yao.

“Tunaiomba Serikali itusaidie kupata mitaji ambayo kupitia mikopo ya riba nafuu ili tuweze kufika mbali na kutoa fursa za ajira kaa watu wengi zaidi,” amesema Denis Joseph ambaye ni mfugaji wa kuku

 

Akijibu hoja hiyo, Katibu mkuu huyo amesema atahakikisha pia anazungumza na katibu mkuu wa Tamisemi ili asilimia kumi inayotengwa katika kila halmashauri iweze kunufaisha wafugaji wadogo ikiwamo wakina mama na vijana.

Kwa sasa sheria inazitaka halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ili kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.

 

 

Advertisement