Serikali ya Tanzania kununua ndege kubwa ya mizigo

Raisi John Magufuli wa kwanza Kushoto akishuhudia makabidhiano ya Ndege ainaya Bombadier Q 400 katika uwanja wa ndege wa Mwanza Dec 14

Muktasari:

Tanzania inakusudia kununua ndege mpya ya mizigo ambayo pamoja na bidhaa zingine, itatumika kusafirisha maua na mbogamboga kutoka viwanja vya Mwanza, Songwe na Kilimanjaro kwenda nje ya nchi hiyo iliyoko barani Afrika.

Mwanza. Serikali ya Tanzania inapanga kununua ndege ya mizigo itakayosafirisha shehena ya bidhaa za maua na mbogamboga kwa lengo la kuongeza fursa za uwekezaji na biashara kwa wakulima nchini humo.

Mapango huo unaokusudia kuongeza na kuimarisha sekta ya usafirishaji kwa njia ya anga ndani na nje ya Tanzania utawezesha safari za moja kwa moja za bidhaa hizo kwenda na kutoka nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumamosi Desemba 14, 2019 katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza kunakofanyika shughuli ya mapokezi ya ndege aina ya Bombardier Q-400 inayotoka nchini Canada.

Amesema mikakati hiyo ndiyo maana Serikali inajenga vyumba vya barafu vya kuhifadhi maua na mbogamboga katika uwanja wa Mwanza, Songwe na Mbeya.

“Mkakati pia unaendelea wa kukarabati chumba cha kuhifadhi mbogamboga na maua katika uwanja wa ndege ya Kilimanjaro,” amesema Rais Magufuli

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametoa ofa ya kusafiri bure kwa wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) waliokutana jijini Mwanza juzi na jana kwenda Dar es Salaam na Zanzibar kesho Jumapili saa 3 asubuhi.