Serikali ya Tanzania kuzipitia upya sheria usalama barabarani

Muktasari:

izara ya Mambo ya Ndani nchini Tanzania ipo katika mchakato wa kuzipitia sheria za usalama barabarani kwa ajili ya kuziongezea makali

Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Tanzania ipo katika mchakato wa kuzipitia sheria za usalama barabarani kwa ajili ya kuziongezea makali.

Imeelezwa kuwa hilo litafanyika kudhibiti madereva, hasa wa bodaboda ambao kwa kiasi kikubwa wanatajwa kuongoza kwa kuvunja sheria na kusababisha ajali zinazoweza kuepukika.

Hayo yameelezwa na naibu waziri wa wizara hiyo, Hamad Masauni wakati akitoa zawadi kwa wanafunzi na shule za msingi za Zanzibar waliofanya vizuri kwenye  shindano la michoro yenye ujumbe wa usalama barabarani kwa mwaka 2019 linaloendeshwa na kampuni ya Puma Energy Tanzania.

“Madereva wa bodaboda wamekuwa wakiendesha pikipiki kwa kuvunja sheria kwa kuwa wanaona haina meno, ili kuwadhibiti akikamatwa kwa kosa la kuvunja sheria anawekwa mahabusu na kisha anapelekwa mahakamani sheria ichukue mkondo wake,” amesema Masauni.

Amesema katika kuhakikisha suala la usalama barabarani linaheshimiwa wizara ipo kwenye mchakato wa kuangalia upya sheria za usalama barabarani kwa lengo la kuziongezea ukali.

Amebainisha kuwa hilo linafanyika kwa lengo la kukabiliana na watumiaji wa vyombo vya moto na hasa madereva bodaboda aliodai kuwa wengi wanavunja sheria na kusababisha ajali zinazoepukika.

Masauni amesema ajali za barabarani zimeendelea kupungua siku hadi siku, lakini bado kuna changamoto kwa baadhi ya watumiaji wa vyombo vya moto na hasa waendesha bodaboda kuvunja  sheria za barabarani.

Amesema kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani na matumizi sahihi ya barabara ili kupunguza ajali zinazosababisha ulemavu na vifo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania Ltd Dominic Dhanan amesema programu hiyo imehusisha shule tano za msingi za Zanzibar ambazo ni Mwembeshauri, Kisiwandui, Jang’ombe, Nyerere  na  Mkunazini.

“Lengo kubwa la mpango huu ni kuwafanya watoto hawa kuwa na uelewa wa matumizi ya barabara wakiwa bado wadogo. Tunaamini kwa kufanya hivyo tunawaongezea uelewa kuhusu dhima nzima ya usalama barabarani kwa wa Tanzania wengi zaidi.”

"Wanafunzi wasiopungua 6,500 wamepata elimu hiyo ambayo imekwenda sambamba na uchoraji wa michoro inayohamasisha matumizi sahihi ya barabarani na kufuata sheria zilizopo," amesema.