Serikali ya Tanzania pania kufikisha watalii milioni 2.4 mwaka 2022

Muktasari:

  • Wahitimu 144 wamehitimu katika ngazi ya astashahada na stashada ya fani mbalimbali katika mahafali ya 17 ya Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Naibu waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Constantine Kanyashu leo Ijumaa Desemba 13, 2019 amesema Serikali kwa inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni 1.6 hadi milioni 2.4 ifikapo mwaka 2022.

Akizungumza katika mahafali ya 17 ya Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam, Kanyashu ameitaja mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza hifadhi za Taifa, ununuzi wa ndege na kuboresha miundombinu ya vivutio vya utalii.

“Serikali ya awamu ya tano imeendelea na mikakati ya kuongeza watalii. Rais  Magufuli ameongeza hifadhi za taifa kutoka 16 hadi 23 na pia huduma za ukarimu kwa watalii zimeongezwa,” amesema Kanyashu.

“Serikali pia imeboresha miundombinu kwa kujenga barabara na imenunua ndege za kutosha. Kwa sasa tunaimarisha Southern circuit (ukanda wa Kusini), ukanda wa Magharibi na sasa ukanda wa mashariki.”

Akieleza umuhimu wa sekta hiyo, Kanyashu amesema mpaka sasa inachangia pato la fedha za kigeni kwa asilimia 25 na asilimia 17.5 ya pato la ndani (GDP).

“Malengo ya Serikali ni kukuza utalii katika ukarimu. Utalii ni sekta muhimu na ndiyo maana wizara ya maliasili na utalii ni miongoni mwa wizara za kipaumbele. Inazalisha zaidi ajira milioni moja. Tumefikisha watalii milioni 1.6 na tunalenga kufikia watalii milioni 2.4,” amesema Kanyashu.

Hata hivyo, amesema licha ya chuo hicho chenye kampasi tatu za Bustani, Temeke na Arusha kutoa wahitimu, bado wadau wamekuwa wakilalamika watumishi wa sekta hiiyo kutokuwa na ukarimu kwa watalii.

Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Kanyashu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa chuo hicho, Dk Shogo Mlozi alisema kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya uhaba wa vyumba vya madarasa na maktaba, viti na madawati.

“Pia kuna uhaba wa mabweni, gari kwa ajili ya kazi za vitendo vya kazi za utalii, gari la mapishi ya mafunzo ya ukarimu ili bidhaa ziwe za moto kwa wateja na hoteli ya mafunzo ka kampasi ya Arusha,” alisema Dk Mlozi.

Jumla ya wahitimu 144 wamehitimu katika ngazi ya astashahada ya fani ya ukarimu, mapishi na mapokezi, huduma ya chakula na vinywaji na fani ya utunzaji wa vyumba na ufuaji wa nguo na fani ya usafirishaji na utalii.

Pia wapo waliohitimu stashahada ya ukarimu, mapishi na mapokezi, fani ya uokoaji na fani ya usafirishaji na utalii.