VIDEO: Serikali ya Tanzania yaahidi kuyatumia mawazo ya Mufuruki

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kumuenzi kwa mawazo na vitendo mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki hasa kwa kusikiliza maoni ya sekta binafsi yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kumuenzi kwa mawazo na vitendo mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki hasa kwa kusikiliza maoni ya sekta binafsi yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Desemba 10, 2019 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki wakati akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali wakati wa kuaga mwili wa Mufuruki katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).

Amesema Mufuruki alikuwa akisimamia anachokiamini hata kama ni tofauti na ilichokiamini Serikali, kwamba lengo lake ni kuona sekta binafsi inakua.

"Serikali tutaendelea kumuenzi Mufuruki kwa maneno na vitendo hasa  kusikiliza maoni kutoka sekta binafsi ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara hapa nchini," amesema Kairuki.

Amesema Serikali inatambua mchango wake katika kukuza uchumi kwa kutengeneza ajira kwa Watanzania kupitia kampuni yake ya Infotech Investment na Woolworth na kulipa kodi serikalini.

Naibu katibu mkuu ofisi ya makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Joseph Sokoine amesema mbali ya kuwa mfanyabiashara, Mufuruki alikuwa mwana mazingira na alipigania uhifadhi wa mazingira.

Amesema katika kundi la WhatsApp la wahifadhi wa mazingira, Mufuruki alikuwa akichangia kwa kutoa uchambuzi kama mtu aliyesomea masuala ya mazingira.

"Mufuruki alikuwa mwenyekiti wa bodi ya ya Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Mazingira, pengine kutokana na mapenzi yake kwenye mazingira ndio maana Rais John Magufuli alimteua kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo," amesema Sokoine.