Serikali ya Tanzania yafuta mapori tengefu 12, vijiji 920 kuneemeka

Waziri Mkuu  wa Tanzania  Kassim Majaliwa akizungumza na Wanahabari juu ya  utekelezaji wa Maagizo ya Rais John Pombe Magufuli kuhusu Mapendekezo ya kupata ufumbuzi wa Migogoro ya Matumizi ya Ardhi Nchini,Mkutano uliofanyika Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es salaam leo Septemba 23, 2019.


Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumatatu ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri Ikulu jijini Dar es Salaam. Katika kikao hicho, Baraza limepokea taarifa ya kamati iliyoundwa na Rais Magufuli kufuatilia migogoro ya ardhi nchini humo na kutoa mapendekezo ambayo yameridhiwa.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeridhia kufuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 ambayo yamepoteza sifa na imeamua yagawiwe kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na mifugo.

Uamuzi huo umefikiwa leo Jumatatu, Septemba 23, 2019 kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akitoa taarifa mara baada ya kikao hicho, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mawaziri wa kisekta wakiongozwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi walichambua na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi nchini iliyowasilishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha leo Jumatatu.

“Mawaziri walichambua na kubaini vijiji vyenye migogoro ni 975 na siyo 366 kama ilivyotangazwa awali.”

“Baraza limeamua kwamba vijiji 920 vitabaki ndani ya hifadhi, mipaka irejewe upya, vipatiwe vyeti vya ardhi vya kijiji pamoja na kupangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi,” amesema Majaliwa

Amesema orodha ya vijiji hivyo itatangazwa baadaye.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeridhia Misitu ya Hifadhi saba yenye ukubwa wa ekari 46,715 iliyopoteza sifa itolewe kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na mifugo ili kuwaondolea kero za uhaba wa ardhi 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeridhia kumega hifadhi za misitu 14 kwa ajili ya kilimo na mifugo na kufuta mashamba 16 yasiyoendelezwa ili yapangiwe matumizi ya kilimo na mifugo.

“Vijiji 55 vilivyobaki vinaendelea kufanyiwa tathmini ya kina maeneo yaliyobaki ndani ya hifadhi na kuwasilisha mapendekezo yake kwa ajili ya uamuzi. Uchambuzi na taarifa itatolewa,” amesema Majaliwa

Majaliwa amesema orodha ya maeneo ya vijiji, mapori ya wanyama, misitu na mashamba yaliyofutwa itatangwa baadaye

Pia, amesema Baraza limeamua ardhi ya mita 500 zilizotengwa kama buffer zone (eneo kinga) kwenye maeneo ya vijiji vinavyopakana na hifadhi za wanyama ziachiwe vijiji husika na wananchi wasiondolewe kwenye maeneo hayo.

Ameyataja uamuzi mwingine waliyofikiwa kwenye kikao hicho ni Ofisi ya Makamu wa Rais imetakiwa ikamilishe mwongozo utakaobainisha matumizi ya ardhi ndani ya hifadhi ya mita 60 za mito, vyanzo vya maji, maziwa na bahari.

Uamuzi mwingine ni kuzitaka wizara na taasisi zote za Serikali zilinde maeneo yao kwa kuweka alama za kudumu zinazoonekana na kwamba wananchi hawaruhusiwi kuvamia maeneo mapya na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya uvamizi wowote kuanzia leo Jumatatu.

Januari, 2019, Rais Magufuli alitoa maagizo kwa mawaziri nane  wa sekta zinazohusika na matumizi ya ardhi wachambue na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi nchini.

Maagizo hayo yalikuwa ni pamoja na: Kutoviondoa vijiji na vitongoji 366 vilivyomo ndani ya hifadhi; kubainisha maeneo ya hifadhi ambayo yamepoteza sifa ili yaweze kugawiwa kwa wananchi kwa shughuli za ufugaji na kilimo na kuhakiki na kurekebisha mipaka baina ya hifadhi za misitu, wanyama na makazi.

Mengine ni kumega baadhi ya hifadhi za Taifa, mapori tengefu na misitu, kuwagawia wafugaji na wakulima; kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi; Kupitia upya Sheria ya Vyanzo vya Maji inayozungumzia uhifadhi ndani ya mita 60; Kuwasilisha mapendekezo ya kufutwa mashamba yasiyoendelezwa na kugawa kwa wananchi kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo na kuendelea kulinda na kuhifadhi maeneo ya hifadhi za misitu, wanyamapori na vyanzo vya maji.