Serikali ya Tanzania yahubiri umuhimu wa elimu

Sunday September 22 2019

By Kelvin Matandiko Mwananchi

Dar es salaam. Serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Joseph Hasunga amesema Taifa lina kazi ya ziada katika uzalishaji wa nguvu kazi kupitia sekta ya elimu.

Hasunga ametoa kauli hiyo leo Jumapili Septemba 22, 2019 wakati wa ibada ya shukrani katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kimara, Jijini Dar es salaam.

Ibada hiyo maalumu imeongozwa na Mwalimu Christopher Mwakasege aliyezungumzia falsafa ya imani katika maisha ya Ukristo hapa duniani.

Viongozi wageni walioshiriki katika ibada hiyo ni Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dean Chediel Lwiza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliyemwakilisha Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Akson.

Wengine ni  Waziri Hasunga aliyepata nafasi ya kutoa salamu mbele ya mamia ya washarika waliojitokeza.

Hasunga amesema takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mwaka 2017, zinaonyesha zaidi ya asilimia 80 ya wananchi waliokuwa na umri kuanzia miaka 16, walikuwa wameishia elimu ya darasa la Saba.

Advertisement

"Kwa kipindi hicho umri wa miaka 16, walikuwa milioni 27.8. Kati yao asilimia 15 hawakuwa katika mfumo wa elimu na asilimia 62.8 walikuwa wameishia darasa la saba kwa hiyo ukijumlisha unapata zaidi ya asilimia 80 walikuwa wameishia elimu ya darasa la saba, "amesema Hasunga.

"Katika asilimia 20 inayobakia, unatoa asilimia 15 tu ndiyo walikuwa wamefika kidato cha nne, lakini asilimia tano tu ya Watanzania ndiyo waliopata cheti, stashahada au shahada."

Hasunga amewaambia washarika hao takwimu hizo zina tafasiri safari ya Tanzania bado ni ndefu, akiwataka kila mmoja kuhakikisha anakuwa sehemu ya kusaidia Taifa kwa kupeleka watoto shule ili kuzalisha nguvu kazi.

Msingi wa kauli yake unachagizwa na msisitizo wa elimu katika Taifa la Israel ambako Yesu alizaliwa.

Amesema mwaka 2018 alipotembelea Israel aliambia na viongozi wa Taifa kwamba, wao walitilia mkazo elimu Kila Myahudi kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo.

"Mila za Kiyahudi kila mtoto lazima ajue kusoma na kuandika, huku kwetu naamini tunaweza kwa uwezo wa Mungu," amesema.

Awali, Waziri Ndalichako amesisitiza suala la umuhimu wa elimu na ushiriki wa wazazi huku akiweka wazi dhamira ya serikali ya awamu ya tano katika kuzalisha wasomi Kwa manufaa ya Taifa.

Pamoja na ujumbe huo wa serikali, katika sehemu ya mahubiri yake, Mwalimu Mwakasege amefundisha wananchi kuwekeza katika maombi ya kumshukuru Mungu yanayofungua mafanikio zaidi kuliko maombi ya uponyaji.

Advertisement