Serikali ya Tanzania yakamilisha maandalizi uchaguzi wa serikali za mitaa

Muktasari:

Uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24, 2019 utahusisha vijiji 12,319 mitaa 4,264, vitongoji 64,384 wenyeviti wa mitaa, vijiji, vitongoji na wajumbe wa halmashauri wa maeneo hayo watachaguliwa.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, (Tamisemi), Joseph Nyamhanga amesema Serikali ya Tanzania imekamilisha maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019.

Akizungumza leo Ijumaa jijini Dodoma wakati wa kutoa tangazo la uchaguzi huo, Nyamhanga ametaja mambo yaliyokamilishwa ni pamoja na uandishi wa kanuni na nyaraka mbalimbali za uchaguzi huo.

“Tumekamilisha kuandaa kanuni za uchaguzi wa Serikali za mitaa 2019, Kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa mitaa katika mamlaka za miji, kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa serikali za kijiji na kanuni za mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji,” amesema Nyamhanga.

Amesema pia Serikali imeandaa mwongozo wa uchaguzi wa viongozi wa vijiji za mwaka 2019 zitakazosaidia kutoa ufafanuzi kwa 2019.

“Tumeandaa mwongozo wa  elimu ya mpiga kura wa serikali za mitaa. Pia, tumeshafanya uhakiki na kuandaa matangazo ya maeneo ya utawala katika serikali za mitaa kupitia matangazo mawili ya serikali 536 la 19, Julai 2019 Notyisi ya mgawanyo ya Serikali katika,” alisema. 

Amesema katika uchaguzi huo katika uhakiki wa maeneo ya utawala utahusisha vijiji 12,319 mitaa 4,264, vitongoji 64,384 ambavyo viongozi mbalimbali watachaguliwa. 

Mkutano huo uliowatanisha viongozi na watendaji wa mikoa mbalimbali ulilenga kutoa maelekezo ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali ili watekeleze majukumu yao kikamilifu.