Serikali ya Tanzania yalipa matrilioni ya fedha ya madeni kwa miaka minne

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imeeleza mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano, pamoja na mafanikio mengine imelipa madeni yaliyoiva.

Dodoma. Waziri wa Fedha na  Mipango wa Tanzania, Dk Philip Mpango amesema katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi Septemba 2019, Serikali imelipa jumla ya Sh24.499 trilioni kwa ajili ya deni lililoiva la fedha zilizokopwa kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Dk Mpango ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 5, 2019, wakati akiwasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na mwongozo wa maandalizi ya mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/21 bungeni.

Ameyataja baadhi ya mafanikio ya utekelezaji wa mpango huo wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano kwa kipindi cha 2016/17 hadi Septemba 2019/2020 ukuaji wa uchumi.

Amesema uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika kwa kukua kwa wastani wa asilimia 7.0 mwaka 2018 kutoka ukuaji wa asilimia 6.8 mwaka 2017.

Amesema pia mfumuko wa bei umeendelea  kupungua na kufikia asilimia 3.4 Septemba mwaka 2019.

“Kuongezeka kwa mapato ya ndani kutoka wastani wa Sh800 bilioni  kwa mwezi katika mwaka 2016/17 hadi kufikia wastani wa Sh1.292 bilioni kwa mwezi katika mwaka 2018/19 kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika ukusanyaji wa mapato,” amesema.

Aidha, amesema juhudi hizo zimeendelea kuleta mafanikio na mapato ya ndani kwa Septemba 2019 yamefikia Sh1.740 trilioni.

Dk Mpango amesema imelipa mishahara ya watumishi wa Serikali yenye jumla ya Sh22,169.9 bilioni na ililipwa kwa wakati katika kipindi chote cha 2016/17 hadi Septemba 2019.

Ametaja mafanikio mengine ni ujenzi wa barabara 23 za lami zilizoongeza mtandao wa barabara kuu za lami kutoka kilomita 7,646 Juni 2016 hadi kilomita 8,306 Juni 2018 na mtandao wa barabara za mikoa umeongezeka kutoka kilomita 1,398 hadi kilomita 1,756.

Waziri huyo amesema ujenzi wa reli ya kati ya Standard Gauge unaendelea  na ujenzi kati ya Dar es Salaam – Morogoro (km 300) ujenzi umefikia asilimia 63 na Morogoro – Makutupora (km 422) asilimia 16.

Kwa upande wa nishati, waziri huyo amesema uwezo wa kuzalisha umeme katika gridi ya Taifa umeongezeka na kufikia megawati 1,613.52.

Amesema idadi  ya vijiji vilivyounganishiwa umeme imefikia 8,102 kati ya Vijiji 12,268 vya Tanzania Bara ambayo ni sawa na asilimia 66.04.

Amesema utekelezaji wa mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere utakaozalisha MW 2,115 unaendelea.

Dk Mpango amesema jumla ya ndege mpya 11 zimenunuliwa na tayari saba zimeshapokewa.

“Utengenezaji wa ndege moja upo katika hatua za mwisho na inatarajiwa kuwasili nchini kabla ya mwisho wa mwaka huu,” amesema.