Serikali ya Tanzania yamuwekea kigingi Tundu Lissu mahakamani

Mawakili Allute Maghai Lissu na Vicent Lissu wote hao ni ndugu wa Mwanasheria mku wa chadema Tundu Lisu wakijadiliana jambo mahakama kuu kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya kuvuliwa ubunge Tundu lissu Picha na Said Khamis

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imetumia mawakili 16 ikiwasilisha hoja tisa kupinga maombi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ikiiomba kutupilia mbali maombi hayo

Dar es Salaam. Aliyekuwa  mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu nchini Tanzania ameanza kukumbana na vigingi katika harakati zake za kutetea ubunge wake aliovuliwa, baada ya Serikali ya nchi hiyo kumwekea pingamizi la awali katika hatua ya awali kabisa ya harakati zake.

Lssu amefungua maombi Mahakama Kuu ya Tanzania, chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute  Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri la maombi maalum kwa lengo la kupata amri mbalimbali kuhusiana na uamuzi huo wa kuvuliwa ubunge.

Amri hizo kwa mujibu wa hati ya maombi na hati ya maelezo yake ni pamoja na mahakama kumwamuru Spika Job Ndugai awasilishe mahakama taarifa ya kumvua ubunge, aliyoitoa bungeni, ili iweze kuupitia na kisha iamuru kuutengua na kuutupilia mbali.

Nyingine ni mahakama imwamuru Spika ampatie yeye Lissu nakala ya taarifa ya kumvua ubunge, amri ya  kusitishwa kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Maombi hayo yalikuwa yamepangwa kusikilizwa leo Ijumaa Agosti 23, 2019, na Jaji Sirilius Matupa, lakini yamekwama baada ya Serikali ya Tanzania kupitia kwa AG, ambaye ndiye mjibu maombi wa pili, kuibua pingamizi la awali akiiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo bila hata kuyasikiliza.

Pingamizi hilo la awali limebainishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Clement Mashamba, aliyeongoza jopo la mawakili wa Serikali 15 kwa niaba ya wajibu maombi, kabla ya  maombi hayo kuanza kusikilizwa.

Kutokana na pingamizi hilo la awali, mahakama imelazimika kusimamishwa usikilizwaji wa maombi ya Lissu na kusikiliza kwanza, pingamizi hilo la AG, kama ulivyo utaratibu wa kawaida.

Dk Mashamba  ameieleza mahakama kuwa katika pingamizi lao hilo la awali wana jumla ya sababu tisa  za kuyapinga maombi hayo yasisikilizwe na badala yake yatupiliwe mbali.

Sababu hizo za pingamizi ni pamoja na kwamba maombi hayo hayajakidhi matakwa ya kisheria kwa kuwa hakuna uamuzi unaolalamikiwa ambao umeambatanishwa katika maombi haya na kwamba hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo ina kasoro za kisheria.

Pia, wanadai nafuu anazoziomba haziwezi kutolewa kwa kuwa hakuna uamuzi kama huo, na kwamba aliyefungua maombi hayo kwa niaba yake, yaani kaka yake Alute Mughwai  hana mamlaka ya kufanya hivyo kwa kuwa hakuna maelezo kuonesha kuwa amepewa mamlaka hayo.

Mpaka sasa mawakili wa Serikali wanaendelea kuwasilisha hoja zao kwa zamu na baada ya kumaliza, jopo la mawakili wake wanne linaloongozwa na wakili Peter Kibatala atakuwa na kibarua cha kupangua hoja hizo za pingamizi ili kukivuka kigingi hicho.

Mwanasheria huyo Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yuko nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake, jijini Dodoma akitokea bungeni.

Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, huku alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba ya Nchi.

Alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutokuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Katika hati ya kiapo chake  kinachounga mkono maombi hayo, wakili Muhgwai anaelezea mkasa mzima wa tukio na mazingira ya shambulizi dhidi yake na matibabu yake nje ya nchi huku akitaja viongozi wa bunge na wa Serikali waliomtembelea akiwa kwenye matibabu Kenya na Ubelgiji.

Katika hati ya maelezo yake, anadai Spika wakati akichukua uamuzi huo hakumpa sababu za kuchukua uamuzi huo wa kumvua ubunge na kwamba alihukumiwa bila kupewa haki ya kusikilizwa.

Pia anadai kuwa alishindwa kuwasilisha tamko kuhusu mali na madeni kwa kuwa alikuwa katika matibabu hospitalini nje ya nchi na kwamba Spika alikuwa anatambua na au alipaswa kutambua hivyo kuwa alijeruhiwa vibaya wakati wa mapumziko ya vikao vya Bunge.

Anasisitiza kuwa katika muda wa miaka saba ya utumishi wake kama mbunge alitekeleza wajibu na majukumu yake kikamilifu kwa kuhudhuria vikao na kushiriki katika mijadala mbalimbali ndani ya bunge.

Katika hati ya dharura Lissu anaiomba mahakama hiyo isikiliza na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka kwani vinginevyo, Mtaturu ambaye Julai 19 mwaka huu  alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ataapishwa kushika wadhifa huo.

Hivyo anadai atakuwa ameathirika kwa kuwa atapoteza haki zake zote, kinga na maslahi yake yote yanayoambatana na wadhifa wake huo wa ubunge.

SOMA ZAIDI

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi