Serikali ya Tanzania yaokoa Sh9.6 bilioni kuhamia Dodoma

Thursday February 13 2020

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Serikali ya Tanzania  imesema baada ya kufanikisha mpango wake wa kuhamia Dodoma, imeokoa Sh9.6 bilioni.

Fedha hizo ni kodi zilizokuwa zikilipwa na taasisi zake  zilizokodisha majengo mbalimbali kwa ajili ya ofisi.

Akizungumza leo Alhamisi Februari 13, 2020  katibu wa Kikosi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma, Meshack Bandawe amesema baada ya Rais John Magufuli kutoa agizo la kutaka taasisi za Serikali zilizopanga kuhamia katika majengo ya Serikali walifanya tathmini.

Amesema kati ya taasisi 82 walizofanyia tathmini wameshahamisha taasisi 48 katika majengo yaliyoachwa na wizara zilizohamia jijini Dodoma.

“Kwa zoezi hili tuliweza kuokoa Sh9.6 bilioni zilizokuwa zikitumika kulipia kodi katika majengo tuliyoyakodi,” amesema.

Amebainisha kuwa watumishi 280 wa Serikali ndio waliobaki jijini Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali ikiwemo umri wa kustaafu kukaribia pamoja na wagonjwa.

Advertisement

Kuhusu ujenzi wa barabara katika mji wa Serikali, Bandawe amesema ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 40 ameshaanza kazi tangu Februari Mosi, 2020.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo utachukua miezi 18 hadi kukamilika.

Advertisement