Serikali ya Tanzania yasema Januari 2020 taasisi zake marufuku kufanya manunuzi nje ya mfumo wa TANePS

Monday November 11 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema Januari mosi, 2020 hakuna taasisi ya umma, itakayopewa fedha kwa ajili ya kufanya mnunuzi nje ya mfumo rasmi, unaotambulika kisheria.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni kutekeleza maagizo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliyoyatoa Septemba 28, 2019 kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuwa ifikapo Desemba 31, 2019 taasisi zote za umma ziwe zimeunganishwa na mfumo wa manunuzi ya umma kwa njia ya mtandao  (TANePS).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Novemba 11, 2019 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amesema ifikapo Januari mosi, 2020  hakuna taasisi itakayoruhusiwa kununua chochote nje ya mfumo huo.

‘’Nilishatoa waraka wa serikali Oktoba 23, 2019 wenye maelezo haya na leo nasisitiza tena, kama ambavyo waziri aliagiza ifikapo  Desemba 31,2019 taasisi zote ziwe zimeingizwa kwenye mfumo huu, nami naagiza ikifika Januari Mosi kama haumo hautafanya manunuzi,” amesema James.

Amefafanua baada ya maelekezo ya waziri wataalamu wa PPRA wamesambaa nchi nzima kwa ajili ya kutoa mafunzo ya jinsi ya kutumia mfumo huo na hivi sasa wapo mkoani Arusha wakiendelea na kazi hiyo.

Amesema taasisi zote zikijiunga na mfumo huo serikali itapata fedha za kutosha, ambazo zilikuwa zinapotea kupitia ununuzi wa umma.

Advertisement

“Taasisi zote zikiingia kwenye mfumo huu Serikali itaokoa wastani wa Sh34 bilioni katika miaka mitano ya mwanzo.”

“Fedha hizo zinatokana na kupunguza gharama za moja kwa moja za manunuzi kama kutayarisha nyaraka za malipo, kusafiri umbali mrefu kufuata huduma na wakati mwingine kujifungia mahali kutayarisha mchakato wa manunuzi,” amesema James.

Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Leonard Kapongo amesema mara baada ya kupatiwa maagizo na waziri mwenye dhamana waliingia kazini kwa kuongeza nguvu ya kutoa mafunzo kuhusiana na matumizi ya mfumo huo kwa maofisa ununuzi na Tehama wa tasisi za umma.

Amefafanua mafunzo hayo yanafanyika kwa awamu na yanaendelea nchi nzima ambapo kwa sasa wataalamu wa PPRA wapo mkoani Arusha wakifanya shughuli hiyo.

“Taasisi 200 zilizoanza kutumia mfumo wa TANePS hivi karibuni mara baada ya kuunganishwa  kufikia leo zimewasilisha  mipango yao ya manunuzi ya mwaka yenye jumla ya zabuni 11,343 zenye thamani ya takribani Sh11.3 trilioni,” amesema Kapongo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA , Martin Lumbanga amesema ‘’Mfumo wa TANePS  utasaidia kufanya kazi kwa uwazi zaidi na kuliwezesha taifa kupata fedha inayostahili.”

Advertisement