VIDEO: Serikali ya Tanzania yasisitiza kutotoa chakula cha msaada

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amewaraka Watanzania kutumia mvua zinazonyesha kulima na kuachana na kilimo cha mazoea huku akisisitiza kwamba Serikali haitatoa chakula cha msaada.

Mwanza. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesisitiza msimamo wa Serikali wa kutotoa chakula cha msaada kwa wananchi watakaokumbwa na njaa kwa uvivu wa kulima.

“Mvua zinanyesha za kutosha; naamini majaruba ya mpunga yamejaa maji. Tuna ardhi ya kutosha yenye rutuba; kila mtu alime na kuchapa kazi kwa bidii kuzalisha chakula cha kutosha yeye na familia yake na ziada ya kuuza kwa ajili ya mahitaji mengine,” amesema Rais Magufuli leo Jumatano Novemba 27, 2019 akiwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga

Ili kuonyesha msisitizo ya kauli yake Rais Magufuli akaongeza; “Kila mtu afanye kazi. Hata kwenye Biblia imeandikwa asiyefanya kazi na asile na asipokula afe.”

Amewashauri Watanzania kuacha kilimo cha mazoea kwa kuendelea kung’ang’ania mazao ya asili ambayo baadhi hayastahimili ukame unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Tulime mazao yanayostahimili ukame kama uwele na mtama,” ameshauri kiongozi huyo

Msisitizo wa kilimo na kufanya kazi kwa bidii ni kati ya masuala yanayopewa kipaumbele tangu mikutano ya asubuhi ya Rais Magufuli kuanzia wilaya za Igunga na Nzega mkoani Tabora ambako amehutubia asubuhi ya leo Jumatano.