Serikali ya Tanzania yataifisha madini ya Sh42.2 bilioni

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imetangaza mali  zilizotaifishwa kutokana na kesi mbalimbali, yakiwemo madini yenye thamani ya Sh42.2 bilioni yaliyokuwa yanatoroshwa nje ya nchi.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetangaza mali  zilizotaifishwa kutokana na kesi mbalimbali, yakiwemo madini yenye thamani ya Sh42.2 bilioni yaliyokuwa yanatoroshwa nje ya nchi.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Februari 10, 2020 na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga wakati akikabidhi serikalini mali  zilizotaifishwa kutokana na kesi mbalimbali, makabidhiano yamefanyika katika ukumbi wa benki kuu ya Tanzania jijini Dar es salaam.

Biswalo amesema  kwa upande wa madini kilo 397.937 za dhahabu  zenye thamani ya Sh32 bilioni zimetaifishwa zilizokuwa zinatoroshwa na kuikosesha Serikali mapato.

Amesema kati ya hizo kilo 351.36 zenye za  Sh29 bilioni ziliuzwa na fedha alikabidhiwa katibu mkuu Hazina.

“Leo nitakabidhi kwa katibu mkuu Hazina kilo 46.177 za dhahabu za Sh3.3 bilioni ambayo ukijumlisha idadi ya dhahabu ndiyo tunapata kilo 397.”

“Pamoja na dhahabu hizo tulitaifisha madini mbalimbali zikiwemo almasi, Tanzanite, Silver, Ruby madini bati yaliyokamatwa Kagera yalikuwa yanataifishwa kwenda nchi nyingine ambako mwekezaji wake aliitangazia dunia yamechimbwa nchini humo kumbe yanapatikana Tanzania pamoja na madini mengineyo,” amesema,

Biswalo amesema thamani ya madini yote yaliyotaifishwa na faini zilizolipwa na watuhumiwa ni Sh42.2 bilioni pamoja na vitu vingine visivyohamishika na vinavyohamishika.