Serikali ya Tanzania yatangaza ajira madaktari 610

Muktasari:

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imetangaza nafasi za ajira za madaktari 610 watakaofanya kazi katika mamlaka za serikali za mitaa.

Dar es Salaam. Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imetangaza nafasi za ajira za madaktari 610 watakaofanya kazi katika mamlaka za serikali za mitaa.

Tamisemi imeeleza kuwa imetangaza nafasi hizo baada ya kupata kibali cha kuajiri na kuwataka wahitimu wa vyuo vikuu  vinavyotambulika na Serikali kutuma maombi ya ajira kuanzia leo Machi 24, 2020.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Tamisemi leo inaeleza kuwa nafasi hizo ni za madaktari daraja la II au daktari wa meno daraja la II.

Imeeleza kuwa waombaji wa nafasi hiyo wanatakiwa kuwa na shahada ya udaktari wa binadamu au meno kutoka vyuo vikuu vinavyotambuliwa na Serikali, waliomaliza mafunzo ya kazi kwa vitendo kwa muda usiopungua mwaka mmoja na kupata usajili kutoka Baraza la Madaktari Tanganyika.

Sifa za mwombaji wa nafasi hizo kwa mujibu wa Tamisemi ni pamoja na mwombaji awe raia wa Tanzania, awe na umri usiozidi miaka 45, awe na vyeti kamili vya mafunzo ya fani aliyosomea.

Nyingine ni kutokuwa mwajiriwa wa Serikali au mwajiriwa wa hospitali za mashirika ya dini ambaye mshahara wake unalipwa na Serikali, lakini pia asiwe amewahi kuajiriwa Serikalini na asiwe na cheki namba.

Tamisemi imetaja nyaraka ambazo mwombaji wa nafasi hizo anatakiwa kuambatanisha kuwa ni barua ya maombi ya kazi ikieleza mikoa mitatu ambayo mwombaji angependa kupangiwa kufanya kazi katika moja ya halmashauri zake.

 

Pia mwombaji anatakiwa kuambatanisha nakala ya cheti cha kidato cha nne au sita, nakala za vyeti vya taaluma, na nakala ya cheti cha kuzaliwa.

Mwombaji ametakiwa kuambatanisha nyaraka kama nakala ya cheti cha usajili kamili au leseni ya kufanya kazi ya taaluma husika na maelezo binafsi, yakionesha umri, anuani kamili na namba ya simu ya kiganjani, pamoja na anuani au namba za simu za kiganjani za wadhamini wasiopungua wawili.

Tamisemi imeeleza kuwa maombi yote yanatakiwa kutumwa kwa njia ya mtandao  kupitia mfumo wa kielektroniki unaopatikana kupitia anuani ya ajira.

Kuhusu aneo la kazi, Tamisemi imesema waombaji wote wanatakiwa wawe tayari kufanya kazi halmashauri yoyote watakayopangiwa, na pia wawe tayari kufanya kazi na mashirika au taasisi zilizoingia ubia na Serikali.

Tamisemi imesisitiza kuwa waombaji watakaotuma au waliotuma maombi yao ya kazi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hawapaswi kuomba nafasi hizo za kazi.