Serikali ya Tanzania yatoa maelekezo kwa mabalozi, wakuu wa mashirika

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amekutana na mabalozi, makaimu mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na kubadilishana mawazo ikiwamo kupeana maelekezo.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewataka mabalozi, makaimu mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kuzingatia sheria za nchi hiyo na mikataba ya kimataifa ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao nchini kwa ufanisi na ufasaha.

Hayo yamesemwa jana Alhamisi Januari 9, 2020 na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi alipokutana na kufanya kikoa jijini Dar es Salaam na viongozi hao wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania.

Alisema mahusiano ya Tanzania na nchi nyingine yanajengwa katika misingi ya mkataba wa Viena, mkataba wa umoja wa mataifa na sheria mbalimbali hivyo ni vizuri mabalozi kuzingatia taratibu hizo.

"Sisi kama tumesisitiza kuwa ni vyema mabalozi na wawakilishi wa nchi zao wakafuata taratibu, mila pamoja na desturi zilizopo katika mikataba hiyo ili kuhakikisha shughuli zao ndani ya Tanzania zinaendana na kufuatana na mkataba wa Viena, mkataba wa umoja wa mataifa lakini pia kunga, mila na desturi za kibalozi," alisema Profesa Kabudi.

Profesa Kabudi alisema Tanzania kupitia mkutano huo imeanza ukurasa mpya wa mahusiano na uendeshaji wa shughuli za Serikali na balozi pamoja na mashirika ya kimataifa yaliyopo Tanzania.

"Tunapata nguvu mpya baada ya mabalozi wote kueleza kuridhika kwao kwa hali ya juu sana na hatua ambazo Serikali ya Tanzania imechukua kupambana na rushwa, kupambana na ubadhirifu wa mali za umma, hatua ambazo Tanzania imechukua katika kuimarisha makusanyo ya kodi lakini pia kusimamia matumizi ya fedha za ndani pamoja na zile zinazotolewa na nchi mbalimbali katika maendeleo ya Tanzania,"  alisema Profesa Kabudi.

Katika mkutano huo, Profesa Kabudi aliwahamasisha mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa kuhusu kuhamia Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa kuwaeleza maendeleo yaliyofikiwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali muhimu na kwamba wakati umefika wa kuharakisha kuhamia Dodoma kwa wakati muafaka kwa kuwa maendeleo yaliyofikiwa nayatoa fursa ya kuwawezesha wao kuhamia jijini Dodoma.

Kwa upande wake, Kiongozi wa mabalozi hao nchini Tanzania ambaye pia ni Balozi wa Comoro, Dk Ahamada Mohamed aliipongeza Tanzania kwa kuitisha mkutano huo mapema ikiwa ni siku tisa tu tangu kuanza kwa mwaka mpya wa 2020 kwa nia ya kubadilishana mawazo na kusikiliza changamoto za mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa pia kuwaelezea hatua za utekelezaji za masuala ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, John Magufuli jambo linalowapa fursa mabalozi hao kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Naye Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu ambaye pia Kiongozi wa Mabalozi wa Bara la Afrika alisema wao kama mabalozi hawawezi kujua mipango, vipaumbele na changamoto za serikali bila ya kuelezwa na kutaka mikutano ya namna hiyo kufanyika mara kwa mara jambo ambalo linatoa uelewa na mwelekeo wa utendaji kazi wa serikali  na hivyo kusaidia kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kwa kutambua fursa na changamoto zilizopo.

Awali, akiwakaribisha mabalozi katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Tanzania, Dk Faraji Mnyepe aliwataka mabalozi kuhakikisha wanazingatia taratibu na kanuni za nchi ili kuhakikisha shughuli zao ndani ya Tanzania zinaendana na kufuatana na mkataba wa umoja wa mataifa.

"Nawasihi sana tufanye kazi kwa kuzingatia taratibu za nchi pamoja na sheria na mikataba kwa manufaa ya nchi yetu (Tanzania) na nchi zenu ili tuweze kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina yetu kwa maendeleo endelevu," amesema Dk Mnyepe

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Dk Damas Ndumbaro, Mkuu wa Itifaki Balozi, Kanali Wilbert Ibuge, mabalozi 28, makaimu mabalozi 12 na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa 10.