Serikali ya Tanzania yatoa sababu kutetea ndoa za utotoni

Muktasari:

  • Hatima ya umri wa kuolewa sasa imebaki mikononi mwa Mahakama Rufani ambayo inatarajiwa kutoa hukumu ya rufaa ya Serikali inayopinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyobatilisha watoto wa kike kuolewa chini ya miaka 18 na kuamuru Serikali ifanye marekebisho ya Sheria ya Ndoa ili umri wa ndoa uanzie miaka 18.
  • Hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufani ndio itakayokuwa uamuzi wa mwisho na mwongozo wa umri sahihi wa kuingia kwenye ndoa  nchini.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania sasa imeiachia Mahakama ya Rufani hatima ya uamuzi wa umri wa kuolewa, baada ya kumaliza kuwasilisha sababu zake za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyobatilisha kifungu cha Sheria ya Ndoa kinachoruhusu ndoa za utotoni.

Serikali ya Tanzania imewasilisha sababu hizo mahakamani hapo wakati mahakama hiyo iliposikiliza rufaa yake iliyoikata kupinga hukumu hiyo ya Mahakama Kuu, iliyosikilizwa jana Jumatano, Julai, 2019, huku ikiwasilisha jumla ya sababu tano.

Miongoni mwa sababu za Serikali ya Tanzania kupinga hukumu hiyo ya Mahakama Kuu iliyobatilisha ndoa inayofungwa na mtoto wa kike mwenye umri wa chini ya miaka 18, Serikali inadai kuwa lengo ni kuwalinda watoto dhidi ya ngono na kupata watoto nje ya ndoa.

Hukumu hiyo ilitokana na kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mwanaharakati wa Haki za Binadamu na mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Msichana Initiative, linalojihusisha na utetezi wa haki ya mtoto wa kike ya kusoma, Rebeca Gyumi.

Rufaa hiyo imesikilizwa jana na jopo la majaji watatu, Augustine Mwarija (kiuongozi wa jopo), Winfrida Korosso na Dk Mary Lavira, ambapo mawakili wa Serikali na mawakili wa mjibu rufani wamevutana kwa hoja za kisheria na kikatiba huku kila upande ukijaribu kuishawishi mahakama ikubaliane na hoja zake.

Jopo la mawakili wa Serikali lililoongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo, lilidai kuwa Mahakama Kuu ilikosea kubatilisha vifungu namba 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambavyo vinaruhus mtoto wa umri wa chini ya miaka 18 anaweza kuolewa au kuoa.

Kwa upande wake, jopo la mawakili watano wa mjibu rufaa lililoongozwa na Mpale Mpoki, akishirikiana na Alex Mgongolwa, Jebra Kambole, Fulgence Massawe na Mary Richard, lilijitahidi kuishawishi mahakama hiyo kuwa Mahakama Kuu ilikuwa sahihi kuamua hivyo.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote iliahirisha kesi hiyo hadi tarehe ya hukumu ambayo wadaiwa wataarifiwa baada ya kumaliza kuiandika.

Katika kesi hiyo ya msingi namba 5 ya mwaka 2016, Gyumi, alikuwa akipinga vifungu namba 13 na 17 vya sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, vinavyoruhusu mtoto wa kike chini ya miaka 18 kuolewa, akidai kuwa vinakiuka haki ya mtoto wa kike kupata elimu.

Pia alikuwa akidai vifungu hivyo ni kinyume cha Ibara za 12, 13, na 18 za Katiba ya Nchi, zinazotoa haki ya usawa mbele ya Sheria, kutokubaguliwa, kuheshimu utu wa mtu na haki ya uhuru wa kujieleza.

Mahakama Kuu katika hukumu yake ya Julai 8, 2016, iliyotolewa na jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo aliyekuwa Jaji Kiongozi, Shaban Lila (kongozi wa jopo), AmaIsario Munisi na Sakieti Kihiyo ilikubaliana na hoja za mwanaharakati huyo.

Ilisema vifungu hivyo ni batili na ni kinyume cha Katiba kwani mtoto umri chini ya miaka 14 hawezi kuingia katika ndoa maana  hana ufahamu kiasi cha kuweza kujihusisha na mambo ya ndoa.

Pia Mahakama ilisema vifungu hivyo ni vya kibaguzi kati ya mtoto wa kike ambaye anaweza kuolewa akiwa na miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi na mtoto wa kiume ambaye anaruhusiwa kuingia kwenye ndoa akiwa na umri wa miaka 18.

Vilevile ilisema kuwa vinakiuka haki ya kikatiba ya kujieleza kwani ndoa ni uamuzi wa mtu binafsi si uamuzi wa wazazi au mtu mwingine. Aliipa Serikali mwaka mmoja ifanyie marekebisho vifungu hivyo na umri wa kuolewa uanzie miaka 18.

Serikali ya Tanzania haikukubaliana na hukumu hiyo ndipo ikakata rufaa hiyo Mahakama ya Rufani.