Serikali ya Tanzania yazungumzia mpango wa kuboresha mazingira ya biashara

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuondoa tozo, ada na kodi ambazo ni kikwazo katika shughuli za uchumi kama zilivyoainishwa katika mwongozo wa kuboresha mzingira ya biashara (Blue Print).

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuondoa tozo, ada na kodi ambazo ni kikwazo katika shughuli za uchumi kama zilivyoainishwa katika mwongozo wa kuboresha mzingira ya biashara (Blue Print).

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ameyasema hayo leo Jumatano Novemba 13,  2019 wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum (CCM), Najma Murtaza Giga.

Katika swali lake Najma amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kwamba tozo na kodi zimezidi na kusababisha aidha kukosa faida au kusababisha mfumuko wa bei pamoja na upungufu wa wateja.

“Je ni lini Serikali itaondoa kero hizo ili kukuza biashara,” amehoji Najma.

Akijibu swali hilo, Dk Ashatu amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wa kipato.

Amesema kwa kutambua umuhimu huo, Serikali kupitia Bunge imekuwa na utaratibu wa kufanya mapitio ya sheria za kodi pamoja na sheria nyingine zinazosimamia tozo na ada kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji. 

Amesema lengo la maboresho hayo ni kupunguza gharama kwa mlipakodi ya kutafuta mtaalam kwa ajili ya kutengeneza hesabu.

Amebainisha kuwa hatua hiyo ililenga kuchochea ulipaji kodi wa hiari na kuongeza mapato ya Serikali.

Pia, Bunge liliridhia mapendekezo ya kupunguza kiwango cha chini cha kodi kutoka Sh150,000 kwa mwaka hadi Sh100,000.

Amesema Serikali kupitia mkakati wa utekelezaji wa Blueprint imefuta na kurekebisha ada na tozo 54 zilizokuwa zinatozwa na taasisi mbalimbali.

Amesema lengo la kufuta ada na tozo hizo ni kuondoa kero na urasimu, kuwapunguzia mzigo wa kodi wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Amesema Serikali itaendelea kufuta na kupunguza baadhi ya kodi, ada na tozo mbalimbali ambazo ni kikwazo katika shughuli za kiuchumi na kijamii kama ilivyoainishwa  kwenye Blue Print.

Akiuliza swali la nyongeza Najma amesema kumekuwa na mfumuko wa bei hasa katika vyakula kama unga unaotumiwa na watu wengi.

“Serikali ina mkakati gani kuhakikisha bei za bidhaa zinazotumiwa na watu wengi zinapungua ili kuwarahisishia wananchi maisha,”amehoji.

Akijibu swali hilo, Dk Ashatu amesema licha ya mfumuko wa bei kuongezeka hakuna upungufu wa chakula nchini.

“Isipokuwa yapo maeneo hayakupata chakula cha kutosha na  kwa sababu ya ushindani uliopo kumekuwa na ongezeko la bei,” amesema.