Serikali ya Tanzania yazungumzia uwezo wa kubangua korosho

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stela Manyanya akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema viwanda vilivyopo nchini vina uwezo wa kubangua tani 73,010 za korosho, kwa sasa zinazobanguliwa ni tani 50,000 kwa mwaka.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema viwanda vilivyopo nchini vina uwezo wa kubangua tani 73,010 za korosho, kwa sasa zinazobanguliwa ni tani 50,000 kwa mwaka.

Ufafanuzi huo umetolewa kutokana na swali la msingi lililoulizwa na mbunge wa Nanyamba (CCM),  Abdallah Chikota aliyetaka kufahamu viwanda vilivyopo nchini vina uwezo gani wa kubangua korosho.

Akijibu swali hilo naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya amesema kwa sasa Tanzania ina jumla ya viwanda vya kubangua korosho 34, vya kati 18 na vidogo 16.

“Viwanda 18 vikubwa na kati vina uwezo wa kubangua tani 63,400 kwa mwaka na 13 kati yake vinafanya kazi,” amesema.

Amesema kati ya  viwanda vidogo 16, tisa vinafanya kazi na vina uwezo wa kubangua tani 9610 kwa mwaka.

Manyanya amesema viwanda vyote 34 vya korosho vina uwezo uliosimikwa wa kubangua tani 73,010 kwa mwaka na uwezo unaotumika kwa sasa ni tani zisizozidi 50,000.

“Serikali imehamasisha sekta binafsi kuanzisha viwanda vya kubangua korosho, imefanikiwa kuwabadilisha wafanyabiashara wakubwa watatu wa kuuza korosho ghafi kujenga viwanda vya kubangua korosho,” amesema.

Amewataja wafanyabiashara hao kuwa Al Andalus Company Mnazi Mmoja Lindi, Mkemia Agrix Company na Fuzzy intenational Company vyote vya Mkuranga Pwani.

Katika swali la nyongeza, Chikota amesema bado kiwango cha ubanguaji wa korosho ni kidogo kwa sababu kwa msimu uliopita walizalisha tani 312,000.

“Je Serikali iko tayari kutoa vivutio maalum ikiwemo kufuta kodi ili kuongeza viwanda vya ubanguaji wa korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi,”amehoji.

Chikota alitaka kujua kama Serikali iko tayari kuondoa urasimu kwa kuweka utaratibu wa wakulima wadhaminiwe na Amcos ili wapewe pembejeo.

Akijibu swali hilo, Manyanya amesema Serikali imekuwa ikiweka vivutio kwa viwanda vinavyotumia malighafi inayozalishwa nchini kwa kuondoa kodi.

Amesema Rais John Magufuli ameanza kuwaunganisha wawekezaji kwa kuanzisha Wizara ya Uwekezaji.

Kuhusu pembejeo, Manyanya amesema wamechukua ushauri huo watauangalia.