Serikali ya Tanzania yazungumzia vurugu za Afrika Kusini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema hakuna Mtanzania aliyeuawa katika Matukio yanayoendelea nchini Afrika Kusini, huku ikiwapa uhakika raia wa nchi hiyo waishio nchini Tanzania kuwa itawalinda wao na mali zao.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema mpaka sasa hakuna Mtanzania aliyeuawa katika machafuko yaliyotokea nchini Afrika Kusini.

Profesa Kabudi ameyasema hayo leo Jumatano, Septemba 4, 2019 katika hafla maalum ya kuwaaga vijana 100 wanaokwenda nchini Israel kwa ajili ya mafunzo ya kilimo kwa vitendo.

Amesema Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Damas Ndumbaro amekuwa nchini humo kwa ajili ya kufuatilia mambo kadhaa na mpaka sasa hakuna taarifa ya kifo wala madhara kwa Mtanzania yeyote.

"Serikali ya Tanzania inaunga mkono tamko la Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa linalolaani mauaji ya Waafrika yanayoendelea hivi sasa. Taarifa zilizopo mpaka sasa hakuna Mtanzania aliyepata madhara," amesema Kabudi.

Aidha Kabudi amewataka Watanzania kutolipiza kisasi kwa wageni waishio hapa nchini.

"Tutawalinda, wapo salama wao na mali zao zitakuwa salama. Mahusiano kati ya nchi hizi mbili yataendelea," amesema Kabudi.

Amesema Wizara yake ina wajibu wa kuhakikisha inafuatilia na kutoa taarifa sahihi.