Serikali ya Tanzania yazungumzia wakimbizi wa Burundi

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema wakimbizi wa Burundi waliopo nchini humo watarejeshwa kwao baada ya amani kurejea, hakuna atakayelazimishwa.


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema wakimbizi wa Burundi waliopo nchini humo watarejeshwa kwao baada ya amani kurejea, hakuna atakayelazimishwa.

Imesema imefanya mazungumzo na Serikali ya Burundi  na mashirika ya kimataifa kuangalia namna ya kuwarudisha wakimbizi hao.

Ufafanuzi huo umekuja siku chache baada ya baadhi ya wakimbizi kudai wanalazimishwa kurejea kwao.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Novemba 6, 2019 na msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas katika mkutano wake na waandishi wa habari aliokuwa akizungumzia utekelezaji wa miradi mbalimbali.

“Sheria inasema sababu ya kuwa na mkimbizi zinapokwisha anatakiwa arudi kwenye nchi yake, ndio kinachofanyika kwa sasa.”

“Hali ya Burundi ni shwari sasa hivi wanatarajia kufanya uchaguzi. Wapo kwenye michakato mbalimbali na kamati imeundwa  kuangalia watakaporudi kwao wanapokewa namna gani, kuna changamoto gani, wanakwenda wapi na  namna gani wanarudi kwenye jamii waliyotoka,” amesema Dk Abbas.

Ameongeza, “hakuna atakayelazimishwa,  tunawarudisha wakimbizi katika nchi walizotoka na kanuni ya kwanza ni wale walio tayari kurudi, hatuwarudishi tu tumehakikisha kwenye nchi zao kuna mifumo ya kuwapokea.”