Serikali ya Tanzania yazungumzia zuio la mikutano ya siasa

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Hamad Masauni amesema utaratibu wa kuzuia mikutano ya kisiasa isiyofuata sheria na taratibu upo palepale na kwamba vyama vyote vya siasa vinapaswa kusubiri muda wa siasa ufike.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema utaratibu wa kuzuia mikutano ya kisiasa isiyofuata sheria na taratibu upo palepale.

Hayo yamesema leo Jumapili Januari 26, 2020 na Naibu waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni Masauni akiwa visiwani Zanzibar alipokuwa akizungumzia hali ya usalama kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2019 visiwani humo.

Amesema muda wa siasa ukifika Serikali itaruhusu mikutano hiyo yenye lengo la kutoa nafasi wa wanasiasa kuzungumza na wananchi.

“Muda wa siasa ukifika watu wataruhusiwa kuendesha mikutano mbalimbali yenye lengo la kueleza kwa wananchi walichokifanya kwa muda waliopewa nafasi baada ya kuchaguliwa na  kuteuliwa katika nafasi  mbalimbali,” amesema

Kuhusu hali ya usalama kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2019, amesema matukio ya mauaji yamepungua kutoka  40 mwaka 2018 hadi 35 mwaka 2019 huku akisema jitihada zimesaidia kupunguza idadi hiyo.

Amesema Serikali kupitia jeshi la polisi na mamlaka nyingine zinazohusika limeanza harakati za kudhibiti matukio  hayo  yanayosababishwa  na  mambo mbalimbali ikiwemo imani za kishirikina.

Katika matukio ya udhalilishaji amesema yameongezeka  baada ya matukio 35  mwaka 2019, ambapo mwaka 2018 yaliripotiwa matukio 15 na kuongeza kuwa jitihada mbalimbali zinafanyika ikiwepo utolewaji elimu kupitia askari wa Shehia na Ofisi ya Polisi Jamii na wadau.

“Matukio  haya  ya  udhalilishaji  ikiwemo kubaka, kulawiti na kunajisi Serikali tumeyaundia mkakati maalumu ikiwemo kamati maalumu iliyoundwa ikisheheni  wataalamu  wa  udhibiti  uhalifu  kutoka jeshi la polisi wakiwemo  wapelelezi, wataalamu wa madawati ya jinsia, tunataka kuona kadhia hiyo ya udhalilishaji inaisha Zanzibar,” amesema.

Kuhusu dawa za kulevya amesema Jeshi la Polisi Zanzibar kwa kushirikiana na taasisi nyingine za ulinzi na usalama liko mbioni katika kudhibiti biashara hiyo.

“Jeshi liko makini katika kudhibiti mtandao  wa biashara hiyo  ambayo tumeona siku za nyuma vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa wakiharibika kwa dawa za kulevya,  kuna mpango maalumu upo katika utekelezaji na tayari umeanza kutoa matokeo chanya ambapo mwaka 2019 watuhumiwa 496 wamekamatwa.”

“Tumekamata pia cocaine gramu 960.65, heroine kilogramu 10.2 na gramu 806.102, bangi kilogramu 659.6 na gramu 649.775 vijana wetu wamezamia kwenye utafunaji mirungi  lakini nayo tushakamata kilogramu10.6 na gramu 096.648 pamoja na vidonge vya Valium gramu 10.30” amesema Masauni.