Serikali yaeleza inavyozuia kilimo cha mazao marefu mijini

Friday April 3 2020

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema haihamishi wakulima maeneo ya mijini badala yake inazuia wakazi wa maeneo hayo kujishughulisha na kilimo cha mazao marefu.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo ameyasema hayo leo Ijumaa Aprili 3, 2020 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ritta Kabati.
Mbunge huyo alihoji ni sheria gani Serikali inayotumia kuwahamisha wakulima kwenye maeneo ya mijini.
Akijibu swali hilo Jafo amesema kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji namba 8 ya mwaka 2017 na Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999, Serikali haihamishi wakulima kwenye maeneo ya mijini.
Amesema badala yake inazuia wananchi kujihusisha na shughuli za kilimo cha mazao marefu katika maeneo hayo.
Pia, Jafo amesema mazao mafupi kama kilimo cha mikunde yanaruhusiwa kulimwa maeneo ya mijini kwa kuzingatia sheria hiyo.

Advertisement