Serikali yakusudia kufanya mabadiliko ya sekta ya kilimo

Monday December 2 2019

Waziri wa kilimo Japahet Hasunga akizungumza

Waziri wa kilimo Japahet Hasunga akizungumza kwenye hafla ya kuhitimisha mradi wa ubia kwa maendeleo ya mifumo ya uzalishaji endelevu wa mpunga Afrika chini ya jangwa la Sahara iliyofanyika Wilaya mvomero 

By Hamida Shariff, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inakusudia kufanya mabadiliko katika sekta ya kilimo kwa kutunga sera na sheria kwa ajili ya kuyalinda maeneo ardhi  ya kilimo ili  yasitumike kwa mipango mingine kama ya  makazi.

Kauli hiyo imetolewa Jana wilayani Mvomero na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, aliyeambatana na Naibu  Waziri wa Kilimo na Ardhi wa Venezuela, Jose Aguilera Contreras kwenye hafla ya kuhitimisha mradi wa ubia kwa maendeleo ya mifumo ya uzalishaji endelevu wa mpunga Afrika, chini ya Jangwa la Sahara unaotekelezwa kwenye nchi 10 ambapo kwa Tanzania mradi huo unatekelezwa wilayani Mvomero, Kilosa na Kilombero.

Amesema maeneo mengi ya kilimo yamegeuzwa kuwa makazi na kufanya maeneo ya kilimo kupungua wakati idadi ya watu  wanaingia katika kushiriki kilimo ikiwa inaongezeka kwa kasi na hivyo kuhatarisha kupunguza uzalishaji wa chakula hapa nchini.

Waziri Hasunga amesema Serikali itaanza kuratibu mchakato wa kutengeneza sera na sheria ya kulinda maeneo ya kilimo ili kuyafanya yaweze kuendelea kuongeza uzalishaji kupitia kilimo  kwa kuwa mahitaji ya chakula nchini bado ni makubwa.

Naye Balozi wa Venezuela katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, Jesus Manzanilla amepongeza ushirikiano uliopo kati ya nchi yake na Tanzania na kwamba, wataendelea kuisaidia katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta kilimo ili kuinua uchumi na kuongeza ajira.

Akizungumzia mradi huo, Manzanilla amesema umekuwa na mafanikio kwa kusaidia nchi kuongeza uzalishaji kupitia zao la mpunga na kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania hasa katika sekta ya kilimo.

Advertisement

Mratibu wa mradi huo kutoka Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO), Diomedes  Kalisa amesema mradi huo umesaidia jumla ya wakulima 2,600 wakiwamo vijana  baada ya kuanza kutumia mfumo wa kilimo shadidi cha mpunga ambacho ni matokeo ya mafunzo ya vijana 150.

Amesema mradi huo ulianza 2016 na unamalizika Desemba 2019, ulikuwa ukisimamiwa na Wizara ya Kilimo kupitia ushauri wa kitaalamu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa(FAO).

Amesema mradi huo  kwa Tanzania ulilenga kwa wakulima wa Skimu za umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga ambalo kwa sasa limeoneka kuwa la kibiashara na sio chakula peke yake.

 

Aidha  amesema mradi huo  ulilenga kukuza uelewa wa wakulima juu ya umuhimu wa mbegu zilizoboreshwa na namna ya kuzipata na kuwasaidia wakulima vijana kwa kuwagaia pembejeo za kilimo, kununua na kufunga mashine za kukoboa na kufungasha mchele kwa madaraja.

Malengo mengine ni pamoja na kuhamasisha juu ya matumizi sahihi ya mbinu bora za utunzaji wa mazao baada ya mavuno kwa wakulima wadogo ili kupunguza upotevu wa mazao.

Mwakilishi wa FAO nchini Fred Kafeero amesema zao la mpunga bado linategemewa kwa uchumi na Tanzania ni nchi ya pili kwa Afrika kwa kuzalisha zao hilo ikiongozwa na Madagsca.

Advertisement