VIDEO: Serikali yatoa neno kuzuiwa ripoti ya IMF

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akizungumza bungeni alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa  Dunia (IMF), jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Fedha na Mipango amesema Serikali haijazuia kuchapishwa kwa ripoti hiyo ila bado inaendelea na mazungumzo na IMF.

Dodoma. Wiki moja baada ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) kueleza kuwa limezuiwa kuchapisha taarifa ya tathmini ya uchumi wa Tanzania, Serikali imepinga suala hilo.

Akijibu swali la Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka leo, Aprili 23, 2019 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema Serikali haijazuia kuchapishwa kwa ripoti hiyo bali inaendelea na mazungumzo na IMF.

Kauli hiyo imetokana na swali la Mwakajoka kujua kwa nini Tanzania imezuia uchapishaji wa taarifa hiyo.

Mwakajoka aliibua hoja hiyo alipokuwa akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa baada ya IMF kuijuza dunia tangu Aprili 17 ilipotoa taarifa kuwa baada ya kikao chake, Serikali ya Tanzania, imezuia kuchapisha tathmini iliyofanywa wala kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Baada ya taarifa hiyo fupi, vyombo vya habari vya kimataifa viliripoti na baadhi ya wanasiasa pamoja na wanaharakati kujitokeza wakitaka taarifa itolewe ili wananchi wajue mwenendo wa uchumi wao.