VIDEO: Serikali yatoa tahadhari Kimbunga Kenneth, yaandaa msaada

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Ajira, Jenista Mhagama ametoa kauli ya Serikali kuhusu Kimbunga Kenneth ambacho juzi Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imesema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kimbunga hicho kilichopo eneo la Kaskazini Magharibi mwa Kisiwa cha Madagascar kinaambatana na mvua kubwa na upepo mkali

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Ajira, Jenista Mhagama amezitaka taasisi za Serikali na binafsi kufuatilia Kimbunga Kenneth na kujiandaa kutoa msaada wa kibinadamu iwapo kitatokea.

Mhagama ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 25, 2019 akisoma taarifa ya Serikali bungeni kuhusu kimbunga hicho chenye ukubwa wa mwekondasi wa upepo unaozunguka kilomita 160 kwa saa katika Pwani mwa nchi za Tanzania na Msumbiji.

Juzi  TMA ilikitambulisha kimbunga hicho kwa jina la Kenneth, ikisema kufikia saa 3:00 asubuhi jana Jumatano Aprili 24, 2019 kimefikia hatua ya sita na kipo kilomita 600 kutoka Pwani mwa Tanzania na Msumbiji.

Akizungumza bungeni, Mhagama amesema kuna uwezekano mkubwa wa kimbunga na mafuriko kutokea  maeneo ya Pwani na Mtwara na mikoa mingine ya jirani kuanzia usiku wa Aprili  24 na 25, 2019 na kuendelea hadi Aprili 26.

“Hali ya hewa inatarajiwa kuanza kubadilika usiku wa Aprili 24 na kutokea kimbunga chenye upepo wa kasi ya kilomita 130 kwa saa katika uelekeo wa mashariki ya mbali kilomita 175 kutoka Pwani ya Mtwara,” amesema Mhagama na kuongeza:

“Kimbunga hicho kinatarajiwa kuendelea kusogea kuelekea Pwani ya Kusini mwa nchi yetu na kuambatana na mafuriko hasa ikizingatiwa Pwani ya Mtwara na Lindi iko chini ya usawa wa bahari.”

Amesema hali hiyo inatarajiwa kuleta athari ya mtawanyiko wa mafuriko na upepo mkali na kusababisha athari, uharibifu wa makazi, mali, mazao na miundombinu kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari ya Hindi kwa kipindi kifupi.

“Usafiri wa anga, majini na nchi kavu utaathirika kutokana na hali mbaya ya hewa. Serikali inaelekeza mamlaka zote na wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara na jirani kuchukua hatua za tahadhari ikiwamo kuwahamasisha wananchi wanaoishi pembezoni mwa bahari ya Hindi kujiokoa kwa kuondoka,” amesema Mhagama na kuongeza:

“Wanaotoa huduma kando ya ndani ya bahari ya Hindi kama uvuvi, usafirishaji wa majini na anga wasimamishe huduma kwa kipindi hicho kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.”

Waziri huyo ameziagiza kamati za maafa katika ngazi zote  maeneo husika kufuatilia kwa karibu kuhusu kimbunga hicho: “Viongozi wa ngazi zote wachukue na kutoa tahadhari katika mitaa yao juu ya uwapo wa hali hii.”

Amesisitiza: “Naendelea kuelekeza hatua stahiki zinachukuliwa kuhakikisha tunakuwa na hali ya utayari ya kutosha ili kuepusha madhara makubwa ya kimbunga na mafuriko.”

Amesema Serikali kwa kuzingatia sheria ya usimamizi wa maafa namba 7 ya mwaka 2015 na kanuni za usimamizi wa maafa za mwaka 2017, inazitaka kamati za maafa kuanzia ngazi za kijiji hadi mkoa kuhakikisha zinakuwa pamoja katika jukumu hilo.