Sh25 milioni za Exim Benki zanunua vitanda Sekondari ya Mrisho Gambo

Muktasari:

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania, Jaffari Matundu amesema mchango huo ni sehemu ya mpango wa uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaotekelezwa na benki hiyo ukilenga kusaidia jamii.

Arusha. Shule mpya ya sekondari ya Mrisho Gambo, leo Alhamisi 13, 2020, imepokea msaada wa fedha kiasi cha Sh25 milioni kutoka Benki ya Exim Tanzania zitakazotumika kununua vitanda pacha 47.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania, Jaffari Matundu amesema mchango huo ni sehemu ya mpango wa uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaotekelezwa na benki hiyo ukilenga kusaidia jamii.

“Benki ya Exim tunaamini kuwa tunalo jukumu kubwa la kufanya katika kuwezesha mabadiliko chanya katika jamii zinazotuzunguka. Elimu ni kati ya maeneo yetu ya kuzingatia na mpango huu unaendana na mkakati wetu wa kubadilisha maisha ya wanafunzi chini ya mpango wa  ‘Exim Cares’ kupitia vitendo endelevu,” amesema.

Ametoa wito kwa taasisi na wadau mbalimbali nchini kuhakikisha wanawekeza kwenye uwezeshaji wa vijana kupitia elimu kutokana na ukweli kuwa bado wanakabiliwa na changamoto nyingi.

“Tumebaini kuna changamoto zinazoathiri vijana wa leo hususani wanafunzi ambazo zinaweza kuwaongoza kuelekea kwenye tabia zisizokubalika ndani ya jamii. Benki ya Exim, tunaamini kwamba kuna haja ya kuelekeza umakini na kuzingatia uwezeshaji wa vijana kupitia elimu. Tutaendelea kuwekeza katika hili na kutimiza wajibu wetu kwa miaka mingi ijayo,” amesema Matundu.

Ameipongeza Serikali kwa kutoa elimu ya msingi bila malipo kwa watoto wote, hatua ambayo alisema ni msaada mkubwa kwa watoto wanaopitia changamoto mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Mkoa Gambo ameipongeza benki hiyo kwa msaada huo huku akibainisha kuwa umetolewa kwa wakati mwafaka.

“Kupitia msaada huu kutoka benki ya Exim, tutaweza kuwasaidia wanafunzi wetu kukaa hosteli, haswa wale ambao kwa sasa wanatembea umbali mrefu kwenda na kurudi. Sasa wataweza kujifunza vizuri na kutambua ndoto zao za masomo,” amesema Gambo.

Amesema mahitaji ya mradi huo ni vitanda 100 na magodoro na jumla ya gharama ni Sh53.7 milioni.