Shahidi aeleza alivyopata taarifa za mkutano wa Zitto

Tuesday October 22 2019

 

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Albert Kitundu, mkuu wa upelelezi Mkoa wa Morogoro ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi alivyopokea taarifa  kuwa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe anakusudia kufanya mkutano na waandishi wa habari.
Kitundu ambaye awali alikuwa msaidizi wa mkuu wa upelelezi wa kituo cha polisi cha Oysterbay Kinondoni, amedai hayo leo Jumanne Oktoba 22, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati akitoa ushahidi katika kesi ya uchochezi inayomkabili kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo.
Shahidi huyo akiongozwa na Wakili wa Serikali mkuu, Tumaini Kweka  amedai Oktoba 28, 2018 akiwa ofisini  alipokea taarifa kuwa  Zitto anakusudia kufanya mkutano na waandishi wa habari.
"Sikujua mkutano wa aina gani anaufanya ila nilielezwa kuwa utafanyika ofisi za makao makuu ya chama hicho. Nilifuatilia  na kubaini mkutano huo umeruhusiwa,” amesema Kitundu.
Amebainisha kuwa Oktoba 29, 2018 aliitwa na mkuu wa upelelezi wa kituo hicho aliyemueleza kuwa wakati anatekeleza majukumu yake alikutana na watu wakijadili mkutano wa Zitto, kwamba ilionyesha  walichukizwa na hotuba ya mbunge huyo, kupata jazba dhidi ya Serikali.
Amesema kwa maelezo hayo mkuu huyo wa upelelezi alimtaka afungue jalada kuhusu uchochezi.
"Tulimwandikia barua na niliwasiliana na mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Kigoma kumtaka atupatie taarifa kwa hayo yaliyosemwa, alitupa maelezo waliyofanya mahojiano na watu mbalimbali," amedai shahidi huyo.
Kitundu amesema maofisa wa polisi walikwenda nyumbani kwa mbunge huyo, wakamchukua na kwenda naye kituo cha polisi Oysterbay ambako walimhoji na alikubali kufanya mkutano na waandishi wa habari.

Amebainisha kuwa walipotaka maelezo yake, Zitto aliwaeleza kuwa hayupo tayari kuyatoa, kuahidi kufanya hivyo mahakamani lakini alikubali kutoa nyaraka za mkutano baada ya kumwagiza kijana wake kuzifuata.
Baada ya maelezo ya shahidi huyo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 22, 2019.
Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi.
Anadaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 28, 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya ofisi za chama hicho zilizopo Kijitonyama, Dar es Salaam.

Advertisement