VIDEO: Shahidi aeleza alivyoshuhudia Mbowe, viongozi Chadema wakiandamana

Muktasari:

Kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema akiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe imeendelea leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambapo shahidi wa nane ametoa ushahidi wake.

Dar es Salaam. Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Kipolisi Mbagala, Dar es salaam nchini Tanzania, Bernard Nyambari (42) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jinsi alivyoweza kuchunguza na kubaini sababu za viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Chadema kufanya maandamano kutoka katika viwanja vya Buibui hadi eneo la Mkwajuni.

Mwenyekiti wa Mbowe, Freeman Mbowe na viongozi wengine wanane wa chama hicho wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 112/2018 yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi.

Nyambari ambaye ni shahidi wa nane katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi hao ameeleza hayo leo Jumatano Septemba 11,2019 wakati akitoa ushahidi wake.

Shahidi huyo ambaye ni Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi ametoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango, shahidi huyo amedai Februari 16, 2018 majira ya jioni, alipigiwa simu na Mkuu wa Upelelezi wa mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, SSP Kungu Marugu eneo la barabara ya Kawawa, ambapo kulikuwa na maandamano.

"Nilienda eneo hilo kama sehemu ya kufanya upelelezi kujua watu waliokuwa wanafanya maandamano ni kina nani," amedai Shahidi.

Amedai alipofika katika eneo la barabara ya Kawawa, alikuta  kundi kubwa la watu wakiwa wameandamana kuelekea barabara ya Mkwajuni katika kituo cha basi cha mwendokasi.

"Nikiwa eneo hilo kama mpelelezi, nilikuta viongozi kadhaa wa jeshi la polisi wakiongozwa na SSP Gerald Ng'ichi na tayari eneo hilo kulikuwa kumeshaanza kupigwa mabomu hewani," amedai

 

Hata hivyo, Shahidi huyo alihojiwa na wakili wa utetezi Peter Kibatala na baadhi ya mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo.

 

Kibatala: Ni sasa Ofisa wa Polisi anatakiwa kuwa nadhifu?

 

Shahidi: Ni sahihi, ofisa wa Polisi anapaswa kuwa nadhifu.

 

Kibatala: Sasa ni kwa nini  hujavaa vest (fulana ya ndani kabla ya kuvaa  shati).

 

Shahidi: Sijavaa vesti kwa sababu hakuna kifungo cha sheria kinachonielekeza nikivaa nguo  za kiraia lazima nivae vesti.

 

Shahidi: Nikiwa kama Ofisa wa Polisi tena mpelelezi navaa nguo yoyote

 

Kibatala: Kwanini hujachomekea?

 

Shahidi: Sijaamua kuchomekea

 

Kesi hiyo imeahirishwa kwa muda wa dakika 30, baada ya hapo itaendelea tena kwa shahidi huyo kuhojiwa na upande wa utetezi.

 

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni wabunge Esther Matiko (Tarime Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), John Mnyika (Kibamba), Ester Bulaya (Bunda Mjini) na Halima Mdee (Kawe).

Pia, kuna Naibu Katibu Mkuu- Zanzibar, Salum Mwalimu na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

SOMA ZAIDI