Shahidi kesi ya Mbowe, mbunge Chadema waugua ghafla mahakamani

Tuesday July 2 2019

 

By Hadija Jumanne na Daniel Francis, Mwananchi. [email protected]

Dar Es Salaam. Kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani Tanzania cha Chadema, akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe na wenzake, imeshindwa kuendelee baada ya shahidi wa sita katika kesi hiyo kuugua ghafla wakati akitoa ushahidi.

Shahidi huyo mwenye namba  F  5392 Koplo Charles, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ameshindwa kumalizia ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, iliyopo Dar Es Salaam, Tanzania  baada ya kujisikia kizunguzungu.

Shahidi huyo ameieleza Mahakamani hiyo leo Jumanne Julai 2, 2019, wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakamani hiyo, Thomas Simba.

Hata hivyo, kabla ya Koplo Charles kujisikia kizunguzungu, Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche aliugua ghafla tumbo hali iliyopeleka mahakama hiyo kusimama kwa muda, kutoa nafasi kwa mbunge huyo kwenda msalani.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi  kesho Jumatano itakapoendelea na washtakiwa wote  wapo nje kwa dhamana.

Awali, akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, Shahidi amedia ameajiriwa na Jeshi la  Polisi mwaka 2003.

Advertisement

Amedia kwa sasa yupo Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Kitengo cha matukio.

Hata hivyo, shahidi huyo ameshindwa kuendelea na ushahidi baada ya kuieleza Mahakamani hiyo kuwa anajisikia kizunguzungu, hivyo anaomba kupumzika kwa muda.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni

Mbunge waTarime Mjini Esther Matiko;   Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu;  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe,  Halima Mdee, Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche, mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Advertisement