VIDEO: Shahidi kesi ya Zitto aeleza walivyovamiwa na polisi na kushuhudia miili ya watu watatu wakiwa wameuawa

Dar es Salaam. Shahidi wa nane wa upande wa utetezi katika kesi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu walivyovamiwa na polisi na kushuhudia miili ya watu watatu waliokuwa wameuawa.


Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 327 ya mwaka 2018.


Shahidi huyo ambaye anajishughulisha na kilimo na siasa Nassib Kapagila (36) mkazi wa kijiji cha Mpeta Wilaya ya Uvinza ameeleza hayo leo Ijumaa Aprili 3, 2020 wakati akitoa ushahidi.


Akiongozwa na wakili wa utetezi, Jebra Kambole mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahid ameeleza kuwa Oktoba 16,2018 wakiwa katika eneo la Mwandubandu walivamiwa na jeshi la polisi.


Ameeleza kuwa wakati tukio hilo linatokea alikuwepo eneo hilo akijiandaa na msiba uliokuwa umetokea.
"Polisi walivamia majira ya saa 11 alfajiri na kurusha risasi na mabomu pamoja na kuchoma moto nyumba," ameeleza Kapagila.
"Tulikuwa tukikimbia huku na huku, tulisikia mtu akilia akisema jamani nakufa ndugu zangu,"
Shahidi huyo ambaye pi ni katibu wa tawi la Mpeta kupitia chama cha ACT Wazalendo aliendelea kueleza Oktoba 17 asubuhi kulikuwa na utulivu ikapigwa ngoma kwaajili ya kukutanika na kujadili kilichotokea.


Ameeleza Oktoba 18 wakiwa wamekusanyika asubuhi alisikia tena milio ya risasi na mabomu akakimbia eneo hilo na kurudi kijijini Mpeta.
"Siku iliyofuata saa 10 jioni nilirudi shambani ambapo nilikuwa nimeacha zana zangu za kazi, wakati napita porini nilikuta miili ya watu watatu wakiwa wamekufa," ameeleza shahidi huyo.
Aliendelea kueleza baada ya kuona miili ile hakufanikiwa tena kuchukua vifaa vyake, alirudi kijijini Mpeta na kutoa taarifa kwa kiongozi wake wa chama, Shaban Almasi.