Sheikh Ponda asema Lissu anatosha urais

Muktasari:

Katibu wa jumuiya na taasisi za Kiislamu Tanzania,  Sheikh Issa Ponda amesema mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu anafaa kuwa rais wa Tanzania.

 

Dodoma. Katibu wa jumuiya na taasisi za Kiislamu Tanzania,  Sheikh Issa Ponda amesema mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu anafaa kuwa rais wa Tanzania.

Sheikh Ponda ametoa kauli hiyo jijini Dodoma leo Jumamosi Oktoba 17, 2020 katika mkutano wa mgombea huyo baada ya kupewa nafasi ya kuufungua kwa dua na kubainisha kuwa Lissu ndio kiongozi anayefaa kuchaguliwa Oktoba 28,2020.

"Sisi tumeamua kuwa ifikapo Oktoba 28 sote kwa umoja wetu tutampigia kura Lissu ili awe Rais wa Tanzania, naomba tuungane katika safari hii ngumu lakini yenye mafanikio," amesema Sheikh Ponda.

Akihitimisha salamu zake mara baada ya Lissu kuhutubia, amewaambia wananchi kuwa mgombea huyo atashinda kiti hicho.

Lissu alieleza furaha aliyonayo kuungana na Ponda ambaye ni kiongozi shupavu katika kutetea haki za wanyonge nchini huku akisema kiongozi hiyo ameshawahi kupigwa lisasi ingawa hafikii idadi ya risasi alizopigwa yeye Septemba 7, 2017.