Shujaa wa Zimbabwe mkali wa kutupia VPL

Muktasari:

Dube aliyesajiliwa na Azam FC msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Highlanders FC ya Zimbabwe na tangu aanze kukinukisha katika Ligi Kuu Bara, Mzimbabwe huyo amethibitisha Wanalambalamba hawajapoteza fedha zao kumnasa nyota huyo kijana.

Ndani ya muda mfupi, mshambuliaji mpya wa Azam FC, Prince Dube amejitengenezea ufalme ndani ya klabu hiyo, huku akiwakuna mashabiki wengi wa soka nchini kwa umahiri wake wa kucheka na nyavu.

Dube aliyesajiliwa na Azam FC msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Highlanders FC ya Zimbabwe na tangu aanze kukinukisha katika Ligi Kuu Bara, Mzimbabwe huyo amethibitisha Wanalambalamba hawajapoteza fedha zao kumnasa nyota huyo kijana.

Kupitia mechi sita za Ligi Kuu na nyingine alizoitumikia Azam FC hadi sasa ameonyesha ni mshambuliaji wa aina gani, ambaye klabu yake ilikuwa ikimsaka tangu ilipoondokewa na Kipre Tchetche kutoka Ivory Coast.

Mkali huyo, katika mechi sita za Ligi Kuu amefunga mabao sita ikiwa ni wastani wa kila moja bao moja na pia kuasisti mara mbili mbali na mechi za kirafiki alizocheza na kuonyesha uwezo mkubwa.

Dube alimejitengenezea ufalme mapema katika Ligi Kuu Bara kutokana na aina ya mabao anayofunga, kwani ana uwezo wa kufunga kwa kichwa na migumu.

Bao la kirafiki

Dube alianza kuonyesha makeke yake kwenye utupiaji mara baada ya kuichezea kwa mara ya kwanza chake katika mchezo wa kirafiki ambapo alifunga bao pekee lililowazima KMC.

Katika mchezo huo, Dube alifunga bao hilo sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho akipokea pasi kwa Obrey Chirwa na mfungaji huyo akiwa ndani ya 18 alitumia akili tulivu kutumbukiza mpira huo wavuni na kuanza kufungua akaunti yake ya mabao.

Mechi tatu mabao matano

Unaweza ukashangaa, lakini ukweli ni kwamba Dube ni aina ya mshambuliaji halisi ambaye anayejua kuifanya kazi yake kwa kufunga kila anapopata nafasi mbele ya lango la mpinzani.

Dube ameonyesha yeye ni mshambuliaji mzuri kwani katika mechi tano ambazo amecheza ametoa pasi ya mabao mawili katika Ligi Kuu, huku akitumia michezo mitatu tu kufunga jumla ya mabao matano yaliyomweka kileleni kwenye orodha ya wafungaji.

Mshambuliaji huyo alianza kufunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Coastal Union, kisha akafunga bao pekee dhidi ya Tanzania Prisons walipoichapa 1-0 na kumalizia udhia kwenye mchezo wao waliopata ushindi mnono wa mabao 4-2 dhidi ya Nkurukumbi, Kagera Sugar.

Kwa kichwa napo hatari

Dube ni mshambuliaji aliyekamilika kwani kwani anapokuwa yupo ndani ya 18 anaweza kukufunga kwa staili yoyote ile ilimradi tu mpira uende wavuni.

Katika mabao yake matano aliyofunga mpaka sasa amefunga, bao moja kwa kwa kichwa kuonyesha Mzimbabwe huyo sio mtu wa mchezo mchezo.

Bao hilo la kichwa la Dube alilifunga dhidi ya Prisons dakika 90 akiunganisha kwa krosi ya winga Idd Seleman ‘Nado’.

Miguu ya maajabu

Achana na kutupia kwa kichwa, huko kwenye miguu jamaa ndio balaa zaidi kwani hachagui wa kutupia mpira kambani, iwe kulia ama kushoto yeye freshi tu!

Katika mabao yake hayo matano, ukiondoa lile la kichwa, manne yaliyobaki kila mmoja amefunga mawili kupitia miguu yake, yaani mawili kulia na mengine kushoto kuthibitisha anapokuwa kazini hachagui silaha ya kukuadhibia.

Dube alionyesha yeye ni balaa kwa kutumia miguu yote miwili wakati akiiadhibu Coastal Union kwa kufunga mabao yake ya kwanza katika Ligi Kuu msimu huu.

Alianza kwa kufunga kwa mguu wa kushoto akimalizia pasi murua ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kabla ya kufunga la pili kwa mguu wa kulia akimalizia pasi ndefu ya Oscar Masai na kukutana nayo ndani ya boksi na kufanya yake.

Kama unadhani alibahatisha kwa Wagosi utakosea, jamaa alirudia tena kitendo hicho cha kuzitungua timu pinzani kwa miguu yote wakati walipomalizana na Kagera Sugar na kuwafumua mabao 4-2.

Mzimbabwe huyo alifunga mabao mawili, la kwanza likitokana na pasi ndefu ya ndani ya boksi kutoka kwa Obrey Chirwa naye kuunganisha wavuni kwa mhuu wa kulia kisha kuja kuongeza jingine la pili kwa guu la kushoto akiunganisha krosi murua ya Idd Seleman ‘Nado’.

Nje ya boksi

Licha ya Dube kuonekana ni mchezaji hatari akiwa ndani ya 18, lakini hadi sasa ana kazi ya kuthibitishia mashabiki kwamba yeye hata nje ya eneo hilo ni balaa, kwani mpaka sasa haonyesha makali.

Dube anaonekana ni mtamu akiwa ndani ya 18 na sasa ana kibarua hiocho cha kuonyesha haya nje ya 18 ni moto na hilo ataweza kulithibitisha kwenye michezo 12 ya duru la kwanza na mingine 17 ya duru la pili ili kukamilisha jumla ya mechi 34 za timu yake katika msimu wake wa kwanza Azam FC.

Hata hivyo kwa kasi aliyoanza nayo ni wazi inawapa kibarua kizito mabeki wa timu pinzani ambao sasa watatakiwa watambue kuwa Dube sio mtu mzuri anapokuwa yupo ndani ya boksi kwani kumruhusu apokee mpira ndani ya eneo hilo basi wajue atawaliza.

Kwa pasi pia balaa

Mabeki sio kumchunga Dube asiwatie aibu langoni mwao, lakini pia wana kazi ya kuhakikisha hata zile pasi zake matata hapati nafasi ya kuzipiga kuwatengenezea wenzake mabao.

Katika mechi tano za ligi, Dube ametengeneza mabao mawili, akitoa pasi murua kwa Chirwa ambaye naye hakuwa na hiyana zaidi ya kuzikwamisha wavuni na kuwa mabao yake pekee mpaka sasa katika ligi hiyo.

Dube alimtengenezea pasi ya bao Chirwa katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania na kwenye pambano la Kagera Sugar.